Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka wafanyabiashara wa Kariakoo kuchangamkia fursa zitakazotokana na Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika unaotarajiwa kufanyika Januari 27 na 28, 2025.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, Mpogolo amewataka wafanyabiashara wa Kariakoo kujiandaa kuwapokea wageni, wakiwemo marais kutoka nchi mbalimbali za Afrika, ambao watahudhuria mkutano huo au kutuma wawakilishi wao.
“Ninawaomba wafanyabiashara kujiandaa kupokea wageni hawa. Huu ni wakati wa kuifanya Kariakoo kuwa ya kimataifa. Serikali itatoa mabango maalum ya kuhamasisha mkutano huu,” amesema Mpogolo katika Bonanza maalumu lililoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Ameeleza kuwa Kariakoo ni tegemeo kubwa kwa Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam, na taifa kwa ujumla katika ukusanyaji wa mapato. Ameahidi ushirikiano mkubwa kati ya serikali na wafanyabiashara kwa lengo la kuongeza ufanisi wa biashara na ukusanyaji wa kodi.
Mpogolo ameipongeza TRA kwa kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato katika mwaka wa fedha 2023/24 ambapo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilikusanya shilingi bilioni 101, ikilinganishwa na malengo ya awali ya bilioni 81. Amesema kwa kasi hiyo, wanatarajia kuongeza lengo hilo hadi kufikia shilingi bilioni 120 kwa mwaka huu wa fedha.
“Serikali wilayani Ilala itaendelea kushirikiana na TRA na wafanyabiashara wote kwa sababu inatambua umuhimu wa kodi katika maendeleo ya miradi mbalimbali, ikiwemo elimu, afya, na barabara,” ameongeza Mpogolo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, Seveline Mushi, amesema wafanyabiashara wa Kariakoo wataendelea kushirikiana na TRA na serikali kwa kuhakikisha wanatoa kodi kwa wakati ili kuchangia maendeleo ya taifa.
Mkutano huo wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika unatarajiwa kuwa fursa muhimu kwa wafanyabiashara wa Kariakoo kujitangaza na kuimarisha biashara zao kimataifa.