Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa nchini (MSD) kushirikiana na Wabunge kusambaza vifaa tiba ikiwemo vitanda vya kujifungulia katika majimbo yote 214 ya Tanzania Bara.
Waziri Ummy ametoa maelekezo hayo Juni 10.2024 Bungeni jijini Dodoma mara baada ya kujibu maswali ya Wabunge ambapo pia Mwenyekiti wa Bunge Dkt. Joseph Mhagama alihoji juu ya changamoto ya utekelezaji wa maagizo na maelekezo ya viongozi wa serikali kupitia watendaji.
“Katika mwaka wa fedha huu ambao tunakaribia kuumaliza, tumesambaza vitanda vya kujifungulia katika majimbo yote 214 ya Tanzania Bara, nilitoa maelekezo kwa MSD kuwa vitanda hivi vikakabidhiwe kwa Wabunge ili wao waweze kuvipeleka katika Hospitali na vituo mbalimbali” Amesema Ummy.
Amesema kuwa serikali inawajibika kwa wananchi kupitia kwa Wabunge hivyo ni lazima kuhakikisha ushiriki wa Wabunge katika masuala mbalimbali ya miradi inayotekelezwa na serikali katika sekta ya Afya.