Latest Posts

MTANZANIA EDHA AJADILI NA RAIS RUTO UWEKEZAJI WA TZS 960 BILIONI KWENYE SARUJI

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Amson Group, Edha Nahdi, amekutana na Rais wa Kenya, William Ruto katika Ikulu ya Nairobi kwa ajili ya mazungumzo kuhusu uwekezaji mkubwa wa upanuzi wa kiwanda cha saruji cha Bamburi Cement- awa mu wa pili, wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 380 (Zaidi ya Shilingi za Kitanzania bilioni 960).
 
Edha alifanikisha ununuzi wa Kampuni ya Bamburi Cement kwa thamani ya TZS 500 bilioni (Dola za Marekani milioni 182), hatua iliyoandika rekodi kama uwekezaji mkubwa zaidi kufanywa na Mtanzania nje ya nchi.
 
Kwa mujibu wa vyanzo vya kiuwekezaji, uwekezaji huu unazidi ule wa mfanyabiashara Rostam Aziz, aliyekuwa amewekeza nchini Kenya kupitia kampuni yake ya Taifa Gas kwa Dola za Marekani milioni 130 (TZS 338 bilioni).
 
Mkataba wa ununuzi wa Bamburi Cement unatajwa kama uwekezaji mkubwa zaidi wa kibinafsi kutoka kwa kampuni ya Kitanzania nchini Kenya tangu kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977. Uwekezaji huu unaimarisha nafasi ya Amson Group kupanua shughuli zake katika ukanda wa Afrika Mashariki.
 
Katika hatua nyingine, Amson Group imeonesha nia ya kuwekeza zaidi nchini Uganda, baada ya Bamburi Cement kukamilisha uuzaji wa hisa zake 70% katika kampuni tanzu ya Hima Cement kwa kampuni za Sarrai Group na Rwimi Holding, kwa thamani ya takribani Dola za Marekani milioni 84 (TZS 214 bilioni) mnamo Machi 2024.
 
Amson Group, inayomilikiwa na familia ya Nahdi, inafanya biashara katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Zambia, Malawi, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi, na sasa inatarajiwa kuwa mzalishaji mkubwa zaidi wa saruji katika Afrika Mashariki.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!