Meya wa Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara Shadida Ndile amewataka madiwani wa manispaa hiyo kwenda kuhamasisha wananchi wao juu ya ukusanyaji wa fedha ili kutimiza makisio ya rasimu waliyojiwekea kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.
Ndile ameyasema hayo akizungumza Februari 19, 2025 wakati wa kikao cha baraza la madiwani hao ambalo limepitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya shilingi bilioni 33.594 ambapo manispaa hiyo imekisia kukusanya na kutumia fedha hizo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Hata hivyo Ndile amewasisitiza madiwani hao kuzingatia vipaumbele ambavyo kila kata imejiwekea ili kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo lengo mi kuwanufaisha na kupunguza changamoto kwa wananchi.

“Twende tukakusanye tukirudi tutaangalia kila kata kipaumbele chake kwenye upande wa elimu, afya, mazingira tutakwenda kuyafanya lakini haya yote yanawezekana endapo tutakuwa na fedha za kutosha tutazoweza kwenda kutekeleza majukumu haya”, amesema Ndile.
Pia ametumia baraza hilo kuwashukuru wataalamu katika manispaa hiyo kwa kuchakata vizuri mpango huo wa bajeti uliyopitishwa na madiwani hao hivyo ni imani yake kuwa baina ya timu hizo mbili wakienda kushirikiana wataenda kupunguza baadhi ya changamoto.
Diwani wa Kata ya Naliendele, Masudi Dali kupitia kikao hicho ameunga mkono bajeti hiyo na kwamba madiwani hao waendelee na ukusanyaji mapato katika maeneo yao ili waweze kufikia malengo yanayokusudiwa.
