Katika tukio lisilo la kawaida, mwananchi mmoja mkazi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, Wilaya ya Njombe, amekata tamaa baada ya kucheleweshwa kwa mikopo ya asilimia kumi licha ya kukamilisha taratibu zote za uombaji.
Mwananchi huyo, ambaye jina lake limehifadhiwa, alituma ujumbe kwa Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Kissa Kasongwa, akieleza hali yake ya kukata tamaa.
DC Kissa amebainisha tukio hilo wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya mikopo yenye thamani ya Shilingi Milioni 474.9 kwa vikundi 81 vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu, iliyofanyika katika ukumbi wa Kanisa Katoliki Ilangamoto mjini Makambako.
“Wanasema kawia ufike. Kulikuwa na malalamiko mengi kuwa mikopo imechelewa, lakini ninaamini ucheleweshaji huu ulikuwa wa manufaa. Hela hizi zingeingia wakati wa Krismasi, pengine zisingetumika kwa malengo yaliyokusudiwa,” alisema DC Kissa.
Akielezea ujumbe huo wa kukata tamaa, DC Kissa amesema: “Mtu mmoja alinitumia ujumbe siku moja kabla ya Krismasi kuniambia, ‘Mnataka roho yangu!’. Nilimuuliza kwa nini? Akasema, ‘Mkopo umechelewa sana, na kilichobaki hapa ni kufa tu.’ Ujumbe huo nilimuonesha Afisa Maendeleo, na ninafurahi kuwa sasa mikopo hiyo imepatikana wakati sahihi, akili ikiwa tayari kwa kazi.”
Mkuu wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa, huku akitoa wito kwa vikundi vyote vilivyopokea fedha hizo kurejesha kwa wakati ili kudumisha uaminifu na kuepuka marekebisho yanayoweza kufanywa na serikali.
Hafla hiyo pia iliwakutanisha viongozi mbalimbali wa serikali na wawakilishi wa vikundi vilivyonufaika na mikopo hiyo, ambayo inalenga kuinua hali za kiuchumi za wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu katika mji wa Makambako.