Latest Posts

MWENYEKITI WA CHADEMA SIHA ATOA WITO WA UMOJA NA KULINDA TAASISI YA CHAMA

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Imma Saro, ametoa wito wa mshikamano na uzalendo kwa wanachama wa chama hicho, akisisitiza umuhimu wa kulinda taswira ya CHADEMA kama tumaini la Watanzania.

Saro amehimiza wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya CHADEMA na wanachama kuepuka ushabiki wa makundi na badala yake kuweka maslahi ya chama mbele.

“Nimewasikiliza wapambe, nawasihi kwamba hatuna CHADEMA nyingine na hatuna chama kingine ambacho ndicho tumaini la Watanzania,” amesema Saro kwa msisitizo, akiwataka wagombea kufahamu uzito wa taasisi wanayoitumikia.

Akieleza kuhusu umuhimu wa wagombea wawili maarufu wa chama hicho, Freeman Mbowe na Tundu Lissu, Saro amesema, “Habari kubwa kila siku ni hawa watu wawili, na hii ni kwa sababu ni Wanachadema. Kila chombo cha habari ndani na nje ya nchi kinatafuta taarifa kuhusu wagombea hawa wawili. Tafadhali kumbukeni CHADEMA ndio tumaini la Watanzania, fanyeni yote kabisa, ila lindeni taasisi yetu.”

Katika ujumbe wake kwa wapiga kura, Saro amewataka wanachama kutanguliza maslahi ya chama badala ya ushabiki wa mtu binafsi.

“Tufahamu kwamba chama ni kikubwa kuliko Mh. Mbowe na Mh. Lissu,” ameongeza, akisisitiza umuhimu wa kura mbili: moja kwa ajili ya kumchagua Mwenyekiti wa Chama na nyingine kwa ajili ya mgombea urais.

Saro pia amehimiza kuzingatia umoja hata baada ya uchaguzi, akisema, “Kura zikipelea, usihame chama; na ukishinda usiendeleze makundi zaidi, rejesha umoja.”

Kauli hiyo inakuja wakati chama hicho kikiwa katika maandalizi ya uchaguzi wa ndani ambao umekuwa ukizua mijadala mikali miongoni mwa wanachama na viongozi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!