Latest Posts

NDEGE YA KIJESHI YA KOREA KUSINI YADONDOSHA MABOMU KWA BAHATI MBAYA, 7 WAJERUHIWA

Watu saba wamejeruhiwa nchini Korea Kusini, wanne kati yao wakiwa katika hali mbaya, baada ya ndege ya kivita KF-16 kudondosha mabomu nane kwa bahati mbaya katika eneo la makazi ya raia wakati wa mazoezi ya kijeshi. Tukio hilo lilitokea katika jiji la Pocheon, karibu na mpaka wa Korea Kaskazini, na kusababisha taharuki kubwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.

Kulingana na taarifa za awali, ni bomu moja pekee ndilo lililolipuka, huku mabomu mengine saba yakisalia bila kulipuka. Kikosi cha kutegua mabomu kinaendelea na juhudi za kuyaondoa kwa usalama. Serikali ya Pocheon imethibitisha kuwa wakazi wa maeneo jirani wamehamishwa kwa tahadhari zaidi.

Ripoti za vyombo vya habari vya ndani zinaeleza kuwa baadhi ya waathirika wamepata majeraha katika shingo na mabega. Jeshi la Anga la Korea Kusini limeomba radhi kwa tukio hilo na kuahidi kuchunguza chanzo cha ajali hiyo, huku likisisitiza kuwa fidia itatolewa kwa waathirika wote.

BBC inaripoti kuwa athari za mlipuko huo zimesababisha uharibifu mkubwa katika majengo ya makazi, ikiwa ni pamoja na kanisa moja na nyumba kadhaa. Picha kutoka kwa vyombo vya habari vya ndani zinaonesha madirisha yaliyovunjika na paa la kanisa lililoharibika vibaya.

Wizara ya Ulinzi ya Korea Kusini imethibitisha kuwa mafunzo hayo ya kijeshi yalikuwa sehemu ya mazoezi ya pamoja na vikosi vya Marekani. Hili linakuja wakati ambapo mataifa hayo mawili yanatarajia kufanya mazoezi makubwa ya pamoja kuanzia Machi 10 hadi Machi 20, ikiwa ni mara ya kwanza tangu Rais wa Marekani, Donald Trump, arejee Ikulu ya White House.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!