Latest Posts

NONDO: SERIKALI IACHE VITISHO, ISIKILIZE WALIMU WASIO NA AJIRA

Mvutano kati ya Umoja wa Walimu Wasio na Ajira Tanzania (NETO) na serikali umechukua sura mpya baada ya hivi karibuni Jeshi la Polisi kumkamata Katibu wa NETO, Daniel Edger Mkinga, huko Kibaha, siku ya Jumanne, Februari 2025, ambaye ameachiwa kwa dhamana siku ya Jumatano jioni.

Hatua hiyo ilikuja muda mfupi baada ya Mwenyekiti wa NETO, Joseph Kaheza, kukamatwa na baadaye kuachiwa kwa dhamana. Kukamatwa kwa viongozi hawa kumeelezwa na baadhi ya wadau wa elimu na siasa kuwa ni dalili ya serikali kutumia vitisho badala ya majadiliano katika kushughulikia madai ya walimu wasio na ajira.

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo Taifa, Abdul Nondo amehoji sababu ya polisi kuingilia kati suala ambalo tayari lilikuwa limeanza kushughulikiwa kwa njia ya mazungumzo kati ya NETO na serikali. Kwa mujibu wa taarifa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, alikuwa tayari amefungua milango ya majadiliano na NETO kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na TAMISEMI. Licha ya juhudi hizo, polisi wameendelea na ukamataji wa viongozi wa NETO, jambo ambalo limezua maswali kuhusu sababu halisi ya hatua hiyo.

Nondo ameeleza kuwa viongozi wa NETO wamekuwa wakidai kuwa usaili wa walimu ulikuwa na kasoro na mfumo wa sasa wa kufanya mtihani wa dakika 40 wa maswali ya kuchagua hauwezi kupima kikamilifu uwezo wa mwalimu. Pia wanahoji jinsi matokeo yanavyotolewa haraka, wakidai kuwa kuna mapungufu yanayohitaji kurekebishwa. Mbali na hilo, NETO wanapinga utaratibu wa walimu kujitolea kwa muda mrefu katika shule za serikali huku ajira zinapotangazwa na wao kuachwa kwa madai ya kufeli usaili. Wanauliza kwa nini serikali inaruhusu walimu wajitolee kwa miaka mingi badala ya kuwapatia ajira rasmi.

Kwa mujibu wa NETO, kuna uhaba wa walimu takribani 279,202 katika shule za msingi na sekondari, huku zaidi ya wahitimu wa ualimu 146,000 wakiwa bado hawana ajira. Umoja huo unahoji kwa nini serikali haijatumia rasilimali watu iliyopo kutatua changamoto ya uhaba wa walimu shuleni. Pia wanahoji kwa nini awali walimu walikuwa wakiajiriwa bila usaili lakini sasa wamewekewa vigezo vipya vya mchujo.

Nondo amesema kuwa serikali inatakiwa kutoa majibu ya wazi kuhusu maswali haya badala ya kutumia vyombo vya dola kuwatisha viongozi wa NETO.

“Kutumia nguvu hakutatui changamoto zinazowakabili walimu bali kunazidi kuibua maswali zaidi”.  Ameeleza Nondo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!