Rais wa Malawi Lazarus Chakwera amesema serikali yake imewasiliana na majirani na washirika wa maendeleo wa nchi hiyo ili kupata msaada wa kutafuta ndege ya kijeshi iliyokuwa imembeba Makamu wa Rais Saulos Chilima na wengine tisa iliyotoweka Jumatatu asubuhi.
Katika hotuba yake usiku wa manane ili kuhabarisha taifa kuhusu ndege iliyotoweka, Rais Chakwera amesema serikali yake imewasiliana na serikali za Marekani, Israel, Norway na Uingereza ili kupata usaidizi.
Washirika wa maendeleo kulingana na Rais wametoa msaada wao kwa njia tofauti ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia maalumu.
“Ninajua kuwa hii ni hali ya kuhuzunisha, ninajua kwamba sote tuna hofu na wasiwasi, mimi, pia nina wasiwasi. Lakini ninataka kuwahakikishia kwamba nitatumia rasilimali yoyote kwenye nchi hii kuipata ndege hiyo na ninashikilia kila aina ya matumaini kwamba tutawapata manusura,” Alisema Chakwera.
Ndege iliyombeba Makamu wa Rais iliondoka katika mji mkuu wa taifa hilo Lilongwe siku ya Jumatatu kuelekea mji wa Kaskazini mwa nchi wa Mzuzu ambako alipangiwa kuhudhuria hafla ya mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo Ralph Kasambara ambaye alifariki ghafla siku ya Ijumaa.
Lakini kwa mujibu wa Jeshi la Ulinzi la Malawi ndege hiyo ilishindwa kutua kama ilivyokuwa imepangwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mzuzu kutokana na kutoonekana vizuri na kulazimika kurejea Lilongwe lakini ikatoweka kwenye rada wakati ikielekea mji mkuu.