Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Evans Mtambi, amekuwa Mkuu wa Mkoa wa kwanza nchini kufungua rasmi akaunti katika Benki ya Ushirika Tanzania, kama njia ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha mifumo ya kifedha ya wakulima kupitia ushirika.
Kanali Mtambi ametekeleza hatua hiyo mara baada ya kuzindua Jukwaa la Ushirika la Mkoa wa Mara, lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mwembeni Complex katika Manispaa ya Musoma. Jukwaa hilo limewaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, ushirika, na taasisi za kifedha.
Ameelekeza Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Mara kuchukua hatua madhubuti kukomesha utoroshaji wa mazao kwenda nje ya nchi, akisema ni lazima kila mazao yasafirishwe kwa utaratibu rasmi unaotambulika kisheria. Pia ametoa agizo kwa vyama vyote vya ushirika mkoani humo kuwa ndani ya mfumo wa TEHAMA wa MUVU kabla ya Mei 30, 2025.
“Saidieni wakulima kwa kutatua changamoto zao, na nisisitize tena, vyama vyote ambavyo havijaingia kwenye mfumo wa MUVU vihakikishe vinafanya hivyo kabla ya tarehe 30 ya mwezi huu,” ameongeza.
Hatua hiyo ya Mkoa wa Mara imekuja ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa maono ya Rais Samia, ambaye Aprili 28, 2025 alizindua rasmi Benki ya Ushirika Tanzania na kuchangia shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kuongeza mtaji wa benki hiyo, inayolenga kuwa mkombozi wa wakulima dhidi ya masharti magumu ya benki binafsi.
Benki ya Ushirika inatarajiwa kutoa mikopo nafuu, ushauri wa kifedha, na huduma shirikishi kwa wakulima, hasa wale wa ngazi ya chini kupitia vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) na SACCOS nchini.