Latest Posts

ROSTAM AZIZ AUNGANA NA WATANZANIA KULAANI MAUAJI YA MOHAMED KIBAO, APONGEZA HATUA ZA RAIS SAMIA

Mfanyabiashara maarufu na mwanasiasa wa zamani, Rostam Aziz, ameungana na Watanzania kulaani vikali tukio la kutekwa na kuuawa kwa kiongozi wa Chadema, Mohamed Ali Kibao.
 
Katika taarifa yake ya Septemba 9, 2024, Rostam ameomboleza kifo hicho akisema kuwa mauaji hayo ni tishio kwa misingi ya amani na umoja wa taifa. Akieleza masikitiko yake, Rostam alisema: “Kifo cha Mohamed Kibao ni pigo kubwa kwa harakati za kidemokrasia nchini. Hatuwezi kuruhusu matukio kama haya yaendelee kuvuruga amani ya nchi yetu.”
 
Katika taarifa hiyo, Rostam pia alisifu hatua za haraka zilizochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kulaani na kuagiza uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo huku akiitaka serikali kuhakikisha haki inatendeka na wahalifu wanachukuliwa hatua kali, akisisitiza umuhimu wa taifa kuepuka kuingia katika hali ya vurugu na giza.
 
“Ni muhimu sasa zaidi ya wakati wowote kuungana pamoja kama taifa na kukataa kurudishwa katika zama za giza ambapo maisha ya binadamu yalikuwa hayana thamani. Hatutaki kurudia makosa ya nyuma,”, ameeleza Rostam.
 
Rostam Aziz, aliyewahi kuwa mbunge wa Igunga kwa tiketi ya CCM amekuwa na ushawishi mkubwa katika nyanja za biashara na siasa nchini. Akiwa amejikita zaidi katika sekta ya nishati, mawasiliano, na kilimo, Rostam pia amekuwa akijitokeza mara kwa mara kutoa maoni yake juu ya masuala ya kitaifa.
 
Katika tamko lake, Rostam Aziz ameonesha dhamira ya kushirikiana na Watanzania wote kudumisha amani, utulivu, na utawala bora, huku akishirikiana na serikali katika kulinda haki za raia.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!