Latest Posts

SERIKALI YA RAIS MWINYI IMESHINDWA KUDHIBITI UCHUMI-ACT

Chama cha ACT Wazalendo kimeibua maswali mazito kuhusu ongezeko kubwa la Deni la Taifa la Zanzibar katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Hussein Mwinyi.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania mwezi Disemba 2024, deni hilo limeongezeka kutoka TZS bilioni 887 mwaka 2021 hadi kufikia TZS trilioni 3.6 mwaka 2024.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, deni la Zanzibar limepanda kwa wastani wa asilimia 59 kila mwaka katika kipindi cha miaka mitatu, kiwango kinachotajwa kuwa cha juu mno ukilinganisha na ukuaji wa uchumi wa asilimia 6 pekee kwa mwaka.

ACT Wazalendo kupitia kwa imeeleza kuwa ongezeko hili ni ishara ya kushindwa kwa Serikali ya Awamu ya Nane kusimamia uchumi wa Zanzibar kwa uwazi na ufanisi.

Katika hotuba yake ya hivi karibuni, Rais Mwinyi ameeleza kuwa deni la Zanzibar ni TZS trilioni 1.2 pekee, akikanusha takwimu za Benki Kuu. Hata hivyo siku ya Jumanne ya tarehe 7 Januari 2025, ACT Wazalendo kupitia msemaji wake wa Sekta ya Fedha, Uchumi na Dira ya Maendeleo – Zanzibar, Prof. Omar Fakih Hamad, imeeleza kuwa takwimu rasmi zinaonesha deni limefikia TZS trilioni 3.6, na kuibua maswali kuhusu uwazi wa taarifa za serikali.

“Serikali ya Zanzibar inadaiwa kuelekeza sehemu kubwa ya fedha hizi katika miradi mikubwa ambayo haijatoa matokeo ya moja kwa moja kwa maisha ya wananchi wa kawaida. Badala yake, miradi hii imekuwa chanzo cha mzigo wa kiuchumi, huku gharama zake zikiwa kubwa kuliko faida zinazotarajiwa”, ameeleza Prof. Hamad.

Ripoti za Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinaonesha kasoro katika utekelezaji wa miradi hiyo, ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya fedha na gharama kubwa zinazozidi faida.

ACT Wazalendo imebainisha kuwa wananchi wanabeba mzigo wa riba kubwa kupitia ongezeko la kodi, kupanda kwa bei za bidhaa muhimu, na ukosefu wa ajira.

“Serikali imeshindwa kushughulikia changamoto za kiuchumi zinazowakumba wananchi, kama vile mfumuko wa bei wa bidhaa muhimu, ukosefu wa ajira, na malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi wa sekta ya umma. Badala ya kuwapa matumaini, serikali imewazunguka wananchi wake katika mtego wa madeni makubwa yanayoendelea kuwa mzigo kwa kizazi cha sasa na kijacho”, imeeleza taarifa ya ACT.

Aidha, ACT Wazalendo imetoa rai kwa wananchi kuhoji matumizi ya rasilimali za umma na kuungana kupinga sera za kiuchumi zinazoendelea kuwa mzigo kwa wananchi, huku ikieleza kuwa Zanzibar inahitaji mwelekeo mpya wa kiuchumi na kisiasa unaojali maslahi ya wananchi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!