Serikali kupitia Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) imeanza kutekeleza kanuni ya majengo (Building Code) itakayotumika kwenye majengo mbalimbali nchini ambayo itasaidia kutatua changamoto zitokanazo na majengo.
Hayo yamebainishwa na T’chawi Mike, Mbunifu Majengo kutoka Chama cha Wabunifu Majengo nchini (AAT), mkoani Morogoro katika kikao kazi cha kuandaa rasimu ya kanuni hiyo ambapo amesema kukamilika kwa uandaaji wa kanuni hiyo na kutumika kwake kutapunguza kero na athari mbalimbali zinazosababishwa na ujenzi usiozingatia kanuni.
Ametaja baadhi ya athari mbaya za ujenzi wa majengo usiozingatia kanuni za ujenzi kuwa ni pamoja na uwepo wa majengo yanayokaribisha majanga, ikiwemo kubomoka, kuanguka, majengo kutokidhi viwango vya ujenzi vinavyoruhusu uokoaji pindi hatari zinapotokea.
Mhandishi Innocent Johnbosco wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) amesema, uandaaji wa rasimu ya kanuni hizi za ujenzi wa majengo umezingatia viwango vinavyotakiwa kitaifa na kimataifa, hivyo kutegemewa kuleta matokeo chanya katika maendeleo ya sekta ndogo ya ujenzi wa majengo nchini.
Aidha, Johnbosco ameshauri elimu ya kutosha itolewe kwa watumiaji wa kanuni hiyo kabla ya kuanza kuitumia, ili kuepuka matumizi yasiyofaa yanayoweza kusababisha kuendelea kuwepo kwa changamoto za ujenzi wa majengo usiofaa na kero nyingine zinazoepukika.
Naye Mbunifu wa Majengo kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (FRF) Joseph Ngido amesema wako tayari kushiriki katika kuhakikisha matumizi sahihi ya kanuni hiyo huku Mhandisi kutoka NCC, Magdalena Hyera akisema uratibu huu unaofanywa na Baraza la Taifa la Ujenzi ni utekelezaji wa majukumu yake ya kisheria.