Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, tarehe 9 Oktoba 2024, ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Tabora, huku akiipongeza Wizara ya Ujenzi kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Akizungumza baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo, Dkt. Mpango amezitaka Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi kushirikiana kikamilifu kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na thamani ya fedha inaonekana.
“Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi, mnajukumu la kuhakikisha fedha hizi, ambazo ni za wananchi, zinatumika vizuri kwa manufaa yao kama ilivyokusudiwa,” alisema Dkt. Mpango.
Kuhusu usalama barabarani, Dkt. Mpango ametoa wito kwa madereva na watumiaji wa vyombo vya moto nchini kuzingatia alama za barabarani ili kuepuka ajali. Pia, amewaonya wanaohujumu alama hizo kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alibainisha kuwa ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho umefikia asilimia 72. Alisema jengo la abiria litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 120 kwa wakati mmoja.
“Mheshimiwa Makamu wa Rais, mradi huu pia unahusisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, mnara wa kuongozea ndege, barabara za maingilio, maegesho ya ndege, barabara ya kuingia katika kiwanja cha ndege, maegesho ya magari, uzio wa usalama, na Kituo cha hali ya hewa,” alifafanua Mhandisi Kasekenya.
Serikali pia imeahidi kuendelea kuunganisha barabara za lami katika mikoa ya magharibi ili kuchochea uzalishaji wa mazao na kukuza uchumi wa wananchi.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, alisema ujenzi huo unafanywa na mkandarasi Beijing Construction Engineering Group Co. kutoka China, kwa gharama ya shilingi bilioni 24.6.
Kiwanja cha Ndege cha Tabora kilianzishwa mwaka 1940 na kimekuwa kikiboreshwa mara kwa mara. Kukamilika kwa mradi huu kutaruhusu ndege kubwa zaidi kutumia kiwanja hicho na kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi katika mkoa wa Tabora na ukanda wa magharibi kwa ujumla.