Latest Posts

SERIKALI YATOA MSAADA WA VIFAA NA CHAKULA KWA MANUSURA WA MAFURIKO KATUBUKA

Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu imekabidhi msaada wa vifaa mbalimbali kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwa ajili ya waathirika waliokumbwa na kadhia ya mafuriko katika eneo la Katubuka lililopo kata ya Katubuka Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma.

Mara baada ya kupokea misaada hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu huku akisisitiza kuwa pamoja na misaada hiyo, serikali ilishapeleka wataalam katika eneo hilo kwa ajili ya kufanya utafiti ili kuja na suluhisho la kudumu dhidi ya kadhia hiyo.

 

Amesema Serikali imeendelea kufuatilia kwa karibu na kutoa makatazo kwa jamii kutoendelea kuishi katika eneo hilo pamoja na kuhakikisha waathiriwa na wakazi katika maeneo jirani wanaendelea kuwa salama.

Kirumbe Ng’enda Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini amesema serikali imefanya jambo la kiutu na kuthibitisha kuwa ni sikivu na yenye kujali wananchi wake.

Amesema katika kupata suluhu ya kudumu ya changamoto ya kujaa maji katika eneo hilo, serikali ipo katika hatua za uchunguzi ili iweze kuandaa mpango utakaoleta suluhisho la kudumu.

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dkt. Rashid Chuachua amesema ameipokea misaada hiyo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa na atahakikisha inawafikia wananchi kama ilivyopangwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi anayeshugulikia Operesheni na Uratibu Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Kanali Celestine Masalamado amesema misaada hiyo imekuja kufuatia ombi la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma lililolenga kuongezewa nguvu katika kusaidia kukabiliana na changamoto za wakazi walioathiriwa na mafuriko katika eneo hilo.

Ameitaja misaada iliyotolewa kuwa ni pamoja na mahindi tani 15.6, maharage tani 4.6, magodoro 283, blanketi 283, ndoo 283, na mikeka 283, ambapo jumla ya kaya 283 zenye wakazi 1304 zitanufaika katika kata za Katubuka, Kibirizi na Bangwe.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!