Serikali imezindua kampeni ya Nishati safi ya kupikia katika mikoa ya Kanda ya Ziwa iliyoenda sambamba na ugawaji wa majiko 100 kwa vikundi vya kijamii kama sehemu ya utekelezaji wa kampeni hiyo nchini ili kuleta tija na kuhifadhi mazingira.
Akizungumza wakati akizindua kampeni hiyo Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange ameipongeza Jumuiya ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Kanda Ya Ziwa Victoria (LVRLAC) kwa kuja na kampeni hiyo ambayo imelenga kuunga mkono jitihada za Serikali kuhakikisha hadi ifikapo 2034 wananchi wanatumia nishati safi na salama.
“Kama mnavyofahamu ni dhamira ya Serikali na ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwamba ifikapo mwaka 2034 tunataka kuona Watanzania ambao wanatumia nishati safi badala ya kutumia nishati chafu,” amesema Dk Dugange
Mwenyekiti wa LVRLAC, William Gumbo amesema kampeni hiyo ni maono yaliyotokana na Mtandao wa Wanawake Kanda ya Ziwa waliochini ya jumuiya hiyo katika kuhakikisha lengo la Serikali kufikia 2034 Watanzania wote wanatumia nishati safi na salama.
“Wanawake ndio vinara wa kuhakikisha kwamba suala la uhifadhi kwa maana ya ulinzi wa ziwa letu victoria unaendana sambamba na maono ya Serikali na uhalisia kwa sababu wanawake ndo wadau wakubwa katika maziwa yetu haya wazee wanapoenda ziwani kutafuta kitoweo wao wanabaki mwaloni wanatuuzia kitoweo,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanawake Kanda ya Ziwa ndani ya LVRLAC, Mariam Maftah amesema wazo la kuja na kampeni hiyo ni matokeo ya maoni yaliyotolewa na wanawake hao katika mkutano mkuu uliofanyika mwaka uliopita.
“Mtandao wa Wanawake ndani ya LVRLAC walitoa wazo katika mkutano mkuu wa mwaka jana na kwa bahati nzuri tulipata wadau ambao walituunga mkono kwa ajili ya kulinda mazingira na sera ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutunza mazingira kwa hiyo tumepata haya majiko tunaamini yatawasaidia wanawake,” amesema.
Mbali na kampeni hiyo kuzinduliwa lakini pia Jumuiya hiyo ya LVRLAC imefanya mkutano Mkuu wa 25 ambao umeongozwa na ujumbe mkuu wa ‘Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025, chagua viongozi bora’.
Akizungumzia mkutano huo Katibu Mkuu wa LVRLAC, Billy Brown amesema mbali na kujadili juhudi mbalimbali zinazofanywa na Halmashauri katika kutunza ziwa Victoria pia watajadili tatizo la aina mpya ya magugu maji lililoibuka Ziwa Victoria.
“Moja ya jambo tutakalo jadili leo ni pamoja na Jumuiya hii itashirikiana na wadau mbalimbali katika kushughulikia tatizo ambalo limeibuka la Magugu Maji ambalo limeonekana kuleta kero na usumbufu kwa jamii na ukanda wa ziwa Victoria,” amesema Brown