Taasisi ya Foundation for Disabilities Hope (FDH) ya mkoani Dodoma, imetoa tuzo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) Dkt. Evance Mwase kwa kutambua mchango wake kwa makundi ya watu wenye ulemavu nchini.
Akikabidhi tuzo hiyo Mkurugenzi wa Taasisi ya FDH, Maiko Salali, amesema tuzo hiyo waliyotoa ni ishara ya kutambua kazi kubwa iliyofanywa na STAMICO, kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake kwa watu wenye ulemavu.
Amesema, Dkt. Evance Mwase, amekuwa mstari wa mbele kuwezesha kupitia fursa mbalimbali kwa makundi ya watu wenye ulemavu ili kujikwamua kiuchumi na kuondokana na dhana ya kuwa tegemezi.
“Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dk. Mwase amekuwa mtu wa mfano katika kuwezesha makundi ya watu wenye ulemavu nchini kwa kutoa fursa mbalimbali ikiwemo walemavu kupata uwakala wa kuuza mkaa mbadala unaozalishwa na STAMICO,” amesema.
Kadhalika, amesema kupitia bidhaa hiyo ya mkaa mbadala watu wenye ulemavu, wamepata fursa ya kujipatia kipato na kujikwamua kiuchumi pia mkaa huo umewasaidia wenye ualibino kulinda afya zao kwa kutumia nishati safi ya kupikia.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dk. Mwase, ameshukuru kupatiwa tuzo hiyo na kuahidi kuendelea kushirikiana na makundi yote ya watu wenye ulemavu nchini ili kusiwe na mtu ambaye anaachwa nyuma.
“Rai yangu watu wenye ulemavu msirudi nyuma serikali yetu chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira wezeshi kwa makundi yenu hivyo kila fursa ambayo inajitokeza mjitahidi kuikamata ili kuwa na jamii jumuishi bila kumwacha yeyote kati yetu nyuma,” ameeleza.