Latest Posts

TAKUKURU KAGERA YAOKOA FEDHA ZA WANANCHI WALIODHULUMIWA

Theophilida Felician Kagera.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera imesema imefanikiwa kuokoa kiasi cha Shilingi milioni 2.3 ambacho kilikuwa kimechukuliwa kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa wananchi 9 wa Kijiji cha Bulembo, Kata ya Ibuga, Wilaya ya Muleba.

Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya TAKUKURU Manispaa ya Bukoba, Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera Hajinas Onesphory alisema watu waliodai kuwaunganisha wananchi hao na huduma ya umeme walikuwa wakiwahadaa kwa kutumia jina la kampuni inayoshughulika na miradi ya umeme vijijini, huku wakiomba malipo isivyo halali.

“Wahusika, Patrick Muchunguzi na Revocatus Masanja, walijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu wakitumia jina la kampuni ya NAKUROI INVESTMENT LTM chini ya REA, wakiahidi huduma ya umeme kijijini ambapo hakukuwa hata na mpango wa kupeleka umeme huo,” alieleza Hajinas.

Baada ya uchunguzi wa kina kufanywa kwa ushirikiano kati ya TAKUKURU na vyombo vya sheria, wahusika walibainika na kulazimika kurejesha fedha walizokusanya kinyume cha sheria. Aidha, wamefukuzwa kazi na kampuni husika.

 

TAKUKURU Yazuia Upotevu wa Vifaa vya Milioni 50 Misenyi

Katika hatua nyingine, TAKUKURU mkoani humo imefanikiwa kuzuia upotevu wa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh milioni 50.3 vilivyokuwa vinaelekezwa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Misenyi.

Kwa mujibu wa Onesphory, katika ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma, taasisi hiyo iligundua kuwa kulikuwa na nyaraka zinazoonesha kuwa vigae vya ujenzi vilivyogharimu kiasi hicho cha fedha vilikuwa vimenunuliwa na kupokelewa, lakini kimsingi havikuwasilishwa na mzabuni kwenye eneo la mradi.

“Kutokana na ufuatiliaji wetu, vifaa hivyo sasa vimewasilishwa rasmi na uchunguzi unaendelea kubaini waliokuwa wamehusika kukwamisha usambazaji huo,” alisema.

 

TAKUKURU Yasihi Wananchi Kushiriki Katika Mapambano

TAKUKURU imewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za viashiria vya rushwa, hasa wakati huu ambao nchi inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais.

“Huu ni wakati muhimu wa kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya rushwa. Ushirikiano wenu ndiyo silaha muhimu ya kuilinda nchi dhidi ya wahujumu wa maendeleo,” amesisitiza Onesphory.

Wananchi waliorejeshewa fedha wameshukuru TAKUKURU na mamlaka zote kwa kuwawezesha kupata haki zao, huku wakiahidi kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa pale inapobidi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!