Waandishi wa habari nchini wametakiwa kushikamana na kuandika kwa umoja wakilenga ajenda zenye kuleta mabadiliko chanya katika jamii, hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, ambao bado unakumbwa na changamoto mbalimbali za kisiasa na kijamii.
Wito huo umetolewa na Wakili Onesmo Olengurumwa, Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), wakati wa mafunzo ya siku moja yaliyofanyika Ijumaa Mei 3, 2025 jijini Dar es Salaam kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini, kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani Mei 3, 2025.

“Waandishi mnayo nafasi ya kipekee ya kuleta mageuzi ya kweli kupitia mijadala mnayoibua. Lakini kwa sasa, sauti zenu zimetawanyika sana na hazijielekezi katika mwelekeo mmoja wa kitaifa,” amesema Wakili Olengurumwa.
Amesisitiza umuhimu wa wanahabari kuripoti kwa weledi na kwa kuzingatia sheria, hasa wakati huu wa uchaguzi ili kulinda usalama wao na kuimarisha amani ya nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Kenneth Simbaya, akifungua rasmi mafunzo hayo, amesisitiza wajibu wa wanahabari kuwa mstari wa mbele kuilinda taaluma yao na kulinda haki za jamii kwa kutoa taarifa sahihi na zisizopotosha.

Katika hatua ya kulinda usalama wa wanahabari wakati wa uchaguzi, jaketi maalum 600 za waandishi wa habari (“press jackets”) zilizinduliwa na kusambazwa, kwa lengo la kuwasaidia wanahabari kutekeleza majukumu yao kwenye mazingira yenye changamoto kwa usalama.

“Changamoto za kiuchumi zisiwe sababu ya kupotosha ukweli au kutumiwa kisiasa. Tujenge taifa letu kwa uzalendo na uadilifu,” ameonya Simbaya.
Simbaya amewataka waandishi kutumia kalamu zao kuelimisha jamii na kuwasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi badala ya kuwa chanzo cha migawanyiko au propaganda zisizo na tija.
Katika mafunzo hayo, wanahabari walielezea kufurahishwa na elimu waliyoipata, wakieleza kuwa imewaongezea maarifa na kuwajengea misingi ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi katika kipindi hiki cha uchaguzi. Swalehe Kassim wa B24 Online alisema:

“Mafunzo haya yamenipa mwanga mkubwa juu ya maadili ya uandishi. Tutaacha kupendelea wagombea kwa bahasha, na badala yake tutawatetea wananchi.”
Naye Hagai Daudi, mwandishi kutoka Mlimani Media ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema: “Ni mara yangu ya kwanza kushiriki mafunzo ya aina hii. Yameniimarisha sana. Ningependa THRDC watembelee chuo chetu ili kutoa elimu zaidi.”
Mtandao wa THRDC umeahidi kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari, vilabu vya waandishi na taasisi nyingine za habari ili kuboresha mazingira ya kazi kwa wanahabari nchini.