Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kanda ya Tabora kimefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kukiuka haki ya kikatiba dhidi ya Mohamed Thabiti Nombo, mkazi wa mkoa wa Tabora.
Kesi hiyo, yenye namba 31308 ya mwaka 2024, inasikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa mkoa wa Tabora chini ya Mheshimiwa Gabriel Ngaeje na ilitajwa kwa mara ya kwanza tarehe 7 Januari 2025.
Katika malalamiko yake, Mohamed Nombo amefungua shauri hilo akilalamikia hatua ya TLS kuwasilisha malalamiko kwa Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Tabora dhidi yake, yakimtuhumu kujiingiza katika kazi za uwakili bila kuwa na sifa zinazostahili kisheria.
Kulingana na TLS, Nombo amekuwa akijihusisha na shughuli za uwakili kama vile kuandaa nyaraka za mahakama na kuwakilisha wadaiwa, akidai kutumia nguvu za kisheria, kinyume cha taratibu za uwakili.
Kwa sasa, kesi hiyo inasubiri majibu ya upande wa TLS, ambapo imepangwa kutajwa tena mahakamani hapo tarehe 21 Januari 2025.
Shauri hili linazidi kuibua maswali kuhusu uangalizi wa taratibu za uwakili na haki za kikatiba, huku ikitarajiwa kuleta mwelekeo kuhusu jukumu la TLS katika kusimamia weledi wa mawakili ndani ya kanda hiyo.