Latest Posts

UBUNIFU WA CSR: MANDO WOMEN GROUP YACHANGIA KOMPYUTA NA VITI KWA ELIMU BORA

Kampuni inayojihusisha na shughuli za ukandarasi, Mando Women Group, imekabidhi kompyuta mbili pamoja na viti vitano vyenye thamani ya jumla ya Shilingi Milioni 3.6 kwa Shule ya Sekondari Bwanga iliyopo wilayani Chato, mkoani Geita. Msaada huo umetolewa kama sehemu ya jukumu la kurudisha fadhila kwa jamii (CSR) kwa mujibu wa mwongozo wa serikali.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo, Mkurugenzi wa Mando Women Group, Bi. Nkwimba Hilu, alisema kuwa kampuni hiyo imeamua kutoa msaada huo kwa lengo la kuboresha elimu ya sayansi na kuongeza ufanisi katika ufundishaji wa somo la kompyuta, sambamba na kwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia duniani.

“Tumeona ni wakati muafaka kuwekeza katika elimu ya TEHAMA kwa wanafunzi wetu, ili kuwasaidia kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidijitali,” alisema Bi. Nkwimba Hilu.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Elimu wa Idara ya Sekondari wilayani Chato, Mwl. Paul Chacha, aliipongeza kampuni hiyo kwa moyo wa kujitolea na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuinua kiwango cha elimu.

“Huu ni mfano wa kuigwa kwa wadau wengine wa maendeleo. Tunaishukuru Mando Women Group kwa kutambua umuhimu wa kushirikiana na jamii,” alisema Mwl. Chacha.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Bwanga, Mwl. Ibrahimu Almas, pamoja na Mwalimu wa somo la Kompyuta, Bi. Flora Mashilingi, walisema vifaa hivyo vitasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto zilizokuwepo awali katika ufundishaji wa somo la kompyuta.

“Tulikuwa tunakabiliwa na uhaba mkubwa wa vifaa vya TEHAMA, jambo ambalo liliathiri kwa kiasi kikubwa ufundishaji wa somo hili. Kupatikana kwa vifaa hivi kutaleta mapinduzi makubwa,” alisema Mwl. Almas.

“Ni faraja kwa walimu na wanafunzi. Tunatarajia kuona ongezeko la ufaulu katika somo hili muhimu,” aliongeza Bi. Mashilingi.

Msaada huu unatarajiwa kuwa chachu kwa wadau wengine wa maendeleo kuchangia katika kuinua elimu nchini, hususan katika maeneo ya vijijini.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!