Na Helena Magabe – Tarime
‎Diwani wa viti maalum tarafa ya Ingwe Mheshimiwa Elizabeth Marembera, amehoji iwapo kuna benki ya damu katika vituo vya afya, kufuatia uhaba wa damu katika Kituo cha Afya Nyangoto kilichopo Nyamongo, wilayani Tarime, mkoani Mara hali inayotajwa kusababisha watu kupoteza maisha kutokana na kuchelewa kuongezewa damu hadi ipoe.
‎Marembera alihoji kuhusu mkakati wa upatikanaji wa damu katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya tatu 2024/2025 kilichofanyika Mei 8, 2025, katika Halmashauri ya Nyamwaga, Tarime Vijijini. Alisema damu inatolewa na kusubiriwa ipoe ndipo wagonjwa waongezwe.
‎”Mwenyekiti, naomba usinijibu kisiasa. Wananchi wameshatoa damu lakini wagonjwa wakifika kituo cha afya unaambiwa damu mpaka ipoe. Kuna mkakati gani wa kuhakikisha damu inapatikana muda wote?” alisema Marembera.
‎
‎Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji, Mhe. Tiboche Richard, alikiri kuwepo kwa uhaba wa damu salama katika kituo hicho kutokana na uhitaji mkubwa wa damu lakini kiwango kidogo cha uchangiaji. Aliwaomba madiwani kuhamasisha wananchi kujitolea damu ili kuepusha adha hiyo.
‎Alisema changamoto hiyo ni kubwa kutokana na wingi wa ajali katika barabara ya Nyamongo, na pia kina mama wengi wanaojifungua huhitaji damu. Hivyo madiwani wanatakiwa kuhamasisha hata makundi mbalimbali kujitolea kutoa damu kwenye vituo vya afya ili kuepusha vifo vinavyosababishwa na ukosefu wa damu salama.
‎Akijibu malalamiko ya vikundi kucheleweshewa pesa zao, alisema fedha hizo zimeshatengwa na kupitishwa. Kwa mujibu wa maelezo ya Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, fedha hizo zitaingia kwenye akaunti za vikundi ndani ya wiki hii.
‎
‎Hata hivyo, alimwomba Diwani wa Kata ya Nyarero kupambana kupitia Kamati ya WDC kuhakikisha anapata maji katika zahanati mbili ambazo alizitaja kuwa na ukosefu wa maji, licha ya kuwa mnufaika wa miradi mbalimbali kutoka halmashauri hiyo.
‎Diwani wa Kata ya Sirari, Amos Sagara, alilalamikia mashine za kufulia nguo zilizopelekwa katika Kituo cha Afya Sirari na Kituo cha Afya Nyarwana katika Kata ya Kibasuka, ambazo zimekaa kwa miaka minne bila kutumika licha ya majengo ya kufulia kukamilika.
‎”Tunaelekea kumaliza muda wetu tangu mashine za kufulia nguo za wagonjwa zilivyoletwa. Tumeshajenga majengo ya kutumia, yamekamilika, lakini mashine hazijaanza kutumika; zinaweza kuwa zimeharibika,” alisema Sagara.
‎Diwani wa Kata ya Nyarero, John Mhabasi, alisema kuwa katika kata yake kuna vituo viwili vya afya ambavyo havina maji.
‎Diwani wa Kata ya Regicheri, John Bosco, alihoji kuhusu vikundi vilivyoomba fedha na kuelezwa kuwa tayari ziko kwenye akaunti, lakini hazikuwemo. Alisema ni mara kwa mara vikundi vinaambiwa fedha zimeingia, lakini ukaguzi unaonyesha bado hazijaingia. Diwani wa viti maalum Tarafa ya Ingwe, Mariam Mkono, naye alilalamikia suala hilo kwa upande wa tarafa yake.