Latest Posts

UJENZI WA MATENKI 15 WA TPA KUIMARISHA UFANISI WA BANDARI YA DAR ES SALAAM NA KUPUNGUZA FAINI ZA MELI

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ametembelea mradi wa ujenzi wa matenki maalum ya kuhifadhia mafuta (Oil Terminal) unaotekelezwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) katika wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam. Mradi huu unahusisha ujenzi wa matenki makubwa 15 yenye uwezo wa kuhifadhi lita 378,000 za mafuta na umepewa sifa kubwa kwa utekelezaji wake.

Akizungumza katika ziara hiyo aliyoifanya katika kata ya Tundwi, Profesa Mbarawa amesema kuwa mradi huu utachukua muda wa miaka miwili na utaimarisha ufanisi wa bandari, huku ukipunguza foleni za meli za kupakua mafuta. Alifafanua kwamba, meli moja inatozwa wastani wa faini ya Shilingi milioni 50 kwa siku wakati inaposubiri kupakua mafuta.

Profesa Mbarawa ameeleza kuwa ufinyu wa matenki ya kuhifadhia mafuta ulisababisha wasafirishaji kutozwa faini kubwa, ambapo gharama hizo zilihamishiwa kwa wananchi. “Wakati mwingine meli hulazimika kusubiri kupakua mafuta zaidi ya wiki moja, hali inayowasababishia wasafirishaji shida na faini hizi,” alisema.

Ameongeza kuwa mradi huu unalenga kuboresha ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam na kuwezesha meli kupakua mafuta kwa muda mfupi, hivyo kuimarisha ushindani wa bandari hiyo kimataifa. Aidha, ujenzi wa matenki haya utawezesha usambazaji wa mafuta kwa urahisi zaidi na kuboresha hifadhi ya mafuta kwa usalama wa nchi.

“Nikiwa kama Waziri wa Uchukuzi, nimefurahi kuona mradi huu ukitekelezwa na napongeza uongozi wa TPA kwa juhudi hizi,” aliongeza Profesa Mbarawa. Alisema kuwa ingawa kulikuwa na changamoto hapo awali, mipango thabiti ya bodi na uongozi wa TPA imewezesha kutekelezwa kwa mradi huu.

Akiongelea kuhusu mradi huo, meneja wa mradi huo Injinia Hamis Hassan Mbutu amesema mradi huo unategemewa kumalizika kwa wakati na kuwa na tija kwa bandari hiyo na Serikali kwa ujumla katika kukusanya ushuru.

Awali, akiongea kabla ya kumkaribisha Profesa Mbarawa, Mkurugenzi Msaidizi wa TPA Juma Kijavara amesema mkataba wa ujenzi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 678.6 ulisainiwa rasmi Februari 26, 2024 ambapo tayari Mkandarasi China Railway Major Bridge Engineering Group ameshalipwa kiasi cha shilingi bilioni 9.9 kuanza ujenzi huo.

Akimuelezea Profesa Mbarawa hatua za utekelezaji wa mradi huo, Injinia Wen Hongyuan kutoka China Railway amesema kuwa mradi huo kwa sasa upo katika asilimia 5 ya utekelezaji ambapo tayari kazi ya kusafisha eneo la ujenzi na ofisi za wajenzi zimekamilika.

Akiongelea kuhusu mgawanyo wa matenki hayo, amesema ujenzi huo utahusisha matenki 6 kwa ajili kuhifadhia mafuta aina ya Dizeli, matenki 5 ya kuhifadhia Petroli na matenki matatu kwa ajili ya kuhifadhia mafuta ya kuendeshea ndege.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!