Na Amani Hamisi Mjege.
Shirika la Msichana Initiative limezindua rasmi ripoti ya hali ya haki na ustawi wa wasichana nchini Tanzania kwa mwaka 2023/24, tukio ambalo limefanyika katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam, Jumanne, Oktoba 8, 2024.
Ripoti hiyo inatoa uchambuzi wa kina kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili wasichana nchini, zikiwemo haki ya elimu, ukatili wa kijinsia, na afya ya uzazi.
Dk. Hellen Kijo Bisimba, mwanaharakati wa haki za binadamu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, ameeleza kwamba kumekuwa na maendeleo fulani katika ustawi wa wasichana nchini, lakini changamoto bado ni nyingi.
Dk. Bisimba amesisitiza umuhimu wa elimu kwa wasichana, akisema kuwa elimu ya kijamii na kijinsia ni muhimu sana katika kukabiliana na ukatili wa kingono. amebainisha kwamba wasichana wengi bado hawana ufahamu wa kutosha kuhusu masuala ya afya ya uzazi, hali inayowaweka katika hatari ya kukumbwa na madhara makubwa ya kijamii kama vile mimba za utotoni.
“Kwenye haki za wasichana kwenye hii taarifa (ripoti) msingi mkubwa ni haki ya elimu, ya darasani ni muhimu sana lakini hata ile ya kijamii ni muhimu. Mfano Kwenye ukatili wa kingono ntu apewe elimu namna ya kupambana nao”, ameeleza Dkt. Bisimba.
Aidha, Dk. Kijo-Bisimba ameeleza kwamba kuna changamoto za umbali wa shule na mazingira duni, kama vile vyoo visivyo rafiki kwa wasichana, hususan wakati wa hedhi. Pia ameonya kuhusu kuongezeka kwa usafirishaji haramu wa binadamu, akisema kuwa watoto wengi wanapotea na baadaye kupatikana wakiwa wameuawa, huku viungo vyao vikichukuliwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Msichana Initiative, Rebecca Gyumi, amesema kuwa ripoti hiyo inachambua hali ya haki na ustawi wa wasichana kwa lengo la kutoa ushahidi ambao utaimarisha juhudi za utetezi wa haki za wasichana nchini Tanzania.
Amebainisha kwamba haki ya kupata elimu ni msingi wa haki zingine zote za wasichana, kwani inachangia afya, ushawishi, na sauti yao katika jamii. Hata hivyo, amesema kuwa wasichana wanakabiliwa na changamoto kubwa zinazohusiana na afya ya uzazi na afya ya akili, huku migogoro na ukatili wa kijinsia vikirejesha nyuma maendeleo ya wasichana wengi.
Ripoti hiyo pia imebaini kwamba changamoto ya ukatili wa kijinsia inaendelea kuathiri wasichana kwa kiasi kikubwa. Fundikira Wazambi, mtafiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ameeleza kuwa takwimu zinaonesha wasichana bado wanateseka zaidi kutokana na vitendo vya ukatili wa kingono.
Kulingana na ripoti hiyo, watoto nane kati ya 10 wanaofanyiwa ukatili wa kingono ni wasichana, huku sehemu kubwa ya vitendo hivyo ikifanyika nyumbani na shuleni, ambapo baadhi ya walimu wanatajwa kuwa vinara wa unyanyasaji huo.
“Tumebaini ukatili mwingi unafanywa katika maeneo ya nyumbani lakini pia shuleni ukatili unafanyika na baadhi ya wanaofanya huo ukatili ni walimu, bado mtoto wa kike ananyanyaswa kingono, bado anaombwa rushwa ya ngono na pia wanafanyiwa vitendo vingine mbalimbali ambavyo vinakiuka haki zao za kibinadamu”, ameeleza Fundikira.
Francis Shao, Mkuu wa Kitengo cha Tathmini na Ufuatiliaji wa Msichana Initiative, ameeleza kuwa changamoto za ukatili wa kijinsia zimekuwa zikiongezeka mwaka hadi mwaka. Hata hivyo, alisema kuwa kumekuwa na upungufu mdogo wa matukio ya mimba za utotoni, lakini matukio mengine ya ukatili yameendelea kuongezeka, hususan yale yanayofanyika ndani ya familia. Ameisitiza umuhimu wa kuwekeza kwenye malezi bora ili kuhakikisha wasichana hawapitii vitendo vya unyanyasaji.
Ripoti hii ya Msichana Initiative imekuja wakati muafaka ambapo jamii inahitaji kuimarisha juhudi za kupambana na ukatili dhidi ya wasichana na kuhakikisha wanapata haki yao ya elimu na afya bora. Shao ameitaka jamii kushirikiana zaidi katika kuhakikisha wasichana wanapata fursa sawa na kulindwa dhidi ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa aina yoyote.