Wawekezaji katika sekta mbalimbali mkoani Geita wametakiwa kutoa fursa za mafunzo kwa vitendo kwa vijana wanaohitimu masomo katika kada mbalimbali, ili kuwaongezea ujuzi unaowawezesha kujimudu katika soko la ajira.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa vitendo kwa vijana 47 waliohitimu masomo katika sekta ya uchimbaji wa madini. Amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imeweka mkazo katika kuimarisha programu za kuwajengea vijana ujuzi ili kuwawezesha kujiajiri na kuendesha maisha yao kwa tija.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML), Duran Archery, amewataka vijana hao kutumia vyema fursa waliyopewa kwa kuwa wao ni sehemu muhimu ya maendeleo ya sekta ya madini nchini.