Latest Posts

WANACHAMA WA CCM WAONYWA KUHUSU MAKUNDI YA UHASAMA KABLA YA UCHAGUZI

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa, amewataka viongozi na wanachama wa chama hicho kuepuka makundi ya uhasama na udhaifu wa maamuzi wakati nchi ikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo kwa viongozi wa CCM katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha Kwa Mfipa, Dkt. Dimwa amesema chama kimejiimarisha kwa mikakati ya kisayansi na madhubuti ili kuhakikisha ushindi wa kishindo dhidi ya hila za wapinzani.

“CCM kimejipanga kitaalamu kwa lengo la kuhakikisha tunapata ushindi wa uhakika, huku tukidumisha umoja, mshikamano na nidhamu ya chama,” alisema Dkt. Dimwa.

Amesisitiza kuwa viongozi walioko kwenye mafunzo hayo wanapaswa kuwa madaraja ya mawasiliano ya maagizo ya chama hadi kwenye ngazi za chini, sambamba na kusimamia utekelezaji wa maelekezo kwa vitendo kwa kuzingatia katiba na miongozo ya chama.

Aidha, Dkt. Dimwa aliagiza viongozi hao kushuka hadi kwenye matawi, kuhimiza ulipaji wa ada za uanachama, kuandaa mpango kazi wa kina na kuimarisha jumuiya zote za chama ili kuongeza wanachama na kujiandaa ipasavyo kwa uchaguzi mkuu ujao.

“Msiruhusu maamuzi yenye misingi ya makundi wala hila. Tumieni maarifa haya kuimarisha chama, kuwa mabalozi wa matumaini, mshikamano na maendeleo kama alivyoagiza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” aliongeza.

Katika hotuba yake, Dkt. Dimwa pia alitoa shukrani kwa Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC) kwa kuendeleza ushirikiano wa kihistoria na kusaidia kifedha, kitaaluma na kiufundi katika kufanikisha mafunzo hayo.

CPC iliwakilishwa na Mkufunzi Yao Jianguo na Naibu Mkurugenzi wa CPC-CIE Xu Sujian, wakishirikiana na timu ya wawakilishi wa CPC nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Uongozi, Prof. Marcelina Chijoriga, alisema mafunzo hayo yameandaliwa kwa kina yakiangazia mada 17 ikiwemo uzalendo na maadili ya uongozi. Aliwataja miongoni mwa wakufunzi kuwa ni Prof. Kitila Mkumbo, ambaye atatoa mada kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020–2025, pamoja na kada maarufu Aggrey Mwanri.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!