Zaidi ya asilimia 50 ya wanachama waanzilishi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), shirika ambalo limejipatia sifa kubwa kwa kutetea haki za kijinsia na usawa katika jamii, wamechukua hatua za kisheria dhidi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa madai ya kuingilia shughuli za ndani za TGNP kinyume cha sheria.
Hatua hii imechukuliwa kutokana na barua tatu zilizotolewa na ofisi ya Msajili ambazo wanachama hao wa TGNP wanazielezea kuwa ni ukiukaji wa misingi ya sheria inayosimamia mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa barua ya tarehe 6 Januari 2025, kutoka kwa kampuni ya uwakili ya Law Guards Advocates inayowakilisha wanachama walioanzisha TGNP kwenda kwa msajili huyo, zaidi ya asilimia 50 ya wanachama wa shirika hilo wamesema kwamba Msajili amefanya maamuzi ambayo yamevuruga uhuru wa shirika.
Wakili Jebra Kambole, anayewakilisha wanachama hao, amesema kuwa hatua za Msajili hazina msingi wa kisheria na zinakiuka misingi ya utawala bora na haki asilia.
“Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali inatoa uhuru kwa mashirika yaliyosajiliwa kufanya kazi zao bila kuingiliwa. Tendo la Msajili ni kinyume na sheria na limeathiri maamuzi halali ya wanachama wa shirika.” Ameeleza Kambole.
Katika barua hiyo, wanachama hao wa TGNP wamedai kuwa ofisi ya Msajili ilituma barua tarehe 18 Novemba 2024, ikidai kuwepo kwa mgogoro ndani ya shirika hilo, jambo ambalo wanachama wanalikana. Msajili alifuatilia kwa barua ya tarehe 3 Desemba 2024, akieleza nia ya kuunda kamati ya kusuluhisha mgogoro huo, hatua ambayo wanasema haikuzingatia taratibu zilizopo. Zaidi ya hayo, barua ya tarehe 16 Desemba 2024 kutoka kwa Msajili ilitoa maelekezo ya kuendelea kwa mkataba wa mkurugenzi wa zamani wa shirika licha ya mkataba huo kumalizika, jambo ambalo linapingwa vikali na wanachama wa shirika hilo.
Wanachama wanasema walifanya mkutano wa dharura tarehe 10 Desemba 2024, ulioshirikisha asilimia 90 ya wanachama, ambapo waliidhinisha uteuzi wa mkurugenzi mpya baada ya mkataba wa mkurugenzi wa awali kufikia tamati. Hata hivyo, Msajili anadaiwa kupuuza maamuzi hayo ya kikatiba na kuchukua hatua za kiutendaji zisizo halali.
Wanasheria wa wanachama hao wa TGNP wanasema kuwa hatua za Msajili zimekiuka Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2002, ambayo inahakikisha mashirika hayo yana uhuru wa kiutendaji mara baada ya kusajiliwa.
Wakili Kambole amesisitiza kuwa Msajili hana mamlaka ya kisheria kuingilia maamuzi yaliyofikiwa kwa mujibu wa katiba ya TGNP. Katika barua hiyo, wanasheria hao wameeleza kuwa Msajili pia alikiuka Kanuni za Haki Asilia kwa kushindwa kuzingatia utaratibu unaotakiwa katika kushughulikia masuala ya ndani ya shirika.
Wanachama wa TGNP wanaitaka ofisi ya Msajili kuacha mara moja kuingilia masuala ya ndani ya shirika hilo na kuheshimu maamuzi yaliyofanywa na wanachama wake. Wanachama hao pia wameonya kuwa endapo Msajili ataendelea na hatua zake za uvunjifu wa sheria, watachukua hatua za kisheria dhidi ya ofisi yake.
“Msajili anapaswa kuheshimu sheria na taratibu zilizowekwa. Hatutakubali maamuzi ya kinyume na sheria yanayovuruga utendaji wa TGNP.” Amesema Wakili Kambole.
WanaTGNP wameeleza kuwa haina pingamizi na usimamizi wa kisheria wa Msajili, lakini wanasisitiza kwamba usimamizi huo ufanywe kwa kufuata sheria bila kuvuruga maamuzi halali ya wanachama wa shirika.
Wakili Kambole amehitimisha kwa kusema, “Mashirika yasiyo ya kiserikali yana jukumu kubwa katika maendeleo ya jamii yetu, lakini hayawezi kufanya kazi kwa ufanisi ikiwa ofisi za umma hazitaheshimu sheria.”
Wanachama wa TGNP wanatarajia kuwa Msajili ataacha mwingilio wake na kuheshimu utawala wa sheria ili kuepusha mivutano ya kisheria isiyokuwa ya lazima.