Wananchi wa Kata ya Ruhuhu, Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe, wameiomba serikali kuanza na kukamilisha ujenzi wa shule ya sekondari katika kata hiyo ili kupunguza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 18 kwenda na kurudi shule ya sekondari ya Manda, iliyopo katika kata jirani.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Ludewa, Joseph Kamonga, baadhi ya wananchi, akiwemo Fausta Nyimbo na Veronica Haule, walisema umbali huo unachangia wanafunzi kuchoka, hali inayowafanya washindwe kuzingatia masomo na mara nyingi kulala darasani. Pia walibainisha kuwa ujenzi wa shule ya sekondari katika kata yao utapunguza matatizo mbalimbali, ikiwemo mimba za utotoni.
Afisa Elimu wa Sekondari wa Halmashauri ya Ludewa, Sunday Deogratius, akimwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri, alisema wataalamu tayari wamekagua eneo litakapojengwa shule hiyo, na hatua za awali za ujenzi zimeanza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ludewa, Wise Mgina, alisema halmashauri imetenga shilingi milioni 40 kutoka mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ili kuanza ujenzi wa shule hiyo, na fedha tayari zipo kwenye akaunti ya shule ya sekondari Manda kwa ajili ya ujenzi huo.
Mbunge wa Jimbo la Ludewa, Joseph Kamonga, alisema anatarajia shule hiyo itaanza kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza ifikapo Januari 2025, na aliwaomba wananchi kuwa wavumilivu wakati ujenzi unaendelea.
Katika utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kati ya mwaka 2020/2021 hadi 2024/2025, Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa imepokea jumla ya shilingi bilioni 8.39 kwa ajili ya miradi ya elimu. Halmashauri hiyo ina jumla ya shule za sekondari 30, zikiwemo 20 za serikali na 10 binafsi, zikiwa na jumla ya wanafunzi 10,406 na walimu 385.