Wananchi wa Wilaya ya Tandahimba, Mkoani Mtwara, wamemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwasogezea huduma za kibingwa na bingwa bobezi karibu, na hivyo kuwawezesha kuepuka safari ndefu za kufuata huduma hizo.
Shukrani hizi zimetolewa na baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata huduma kutoka kwa madaktari bingwa walioweka kambi ya siku sita katika halmashauri tisa za mkoa wa Mtwara.
Miongoni mwa wakazi waliopata huduma katika Hospitali ya Mji wa Nanyamba ni Mohammed Issa (29), ambaye alimpongeza Rais Samia kwa hatua hiyo, akibainisha kuwa huduma hizi zimewafikia wananchi wa ngazi ya msingi, ambao kipato chao ni cha chini, na awali walilazimika kusafiri umbali mrefu na kutumia gharama kubwa kupata huduma za kibingwa na bingwa bobezi.
“Hakika, kambi hii ya ujio wa madaktari bingwa wa Mama Samia kutufikia katika maeneo yetu ni ishara ya wazi ya utendaji mzuri na uwajibikaji wa kiongozi wetu kwa wananchi wake, ili kuhakikisha tunakuwa na afya bora kwa ajili ya kuendelea kulitumikia taifa katika shughuli za maendeleo,” alisema Issa.
Kwa upande wake, Bwana Hamisi Malela Mnandaje (47), mkazi wa Wilaya ya Tandahimba, ametoa wito kwa wananchi wenzake kuhakikisha wanakata bima ya afya mara baada ya mauzo ya zao la korosho, ili kuwa na uhakika wa matibabu.
Amebainisha kuwa serikali chini ya uongozi wa Rais Samia imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya, ikiwemo kuhakikisha madaktari bingwa na bingwa bobezi wanafika katika ngazi ya msingi, ili wananchi wapate huduma hizo karibu na maeneo yao.
Aidha, Bwana Mnandaje ametoa wito kwa wananchi wa Mtwara kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kutolea huduma za afya vilivyotangazwa, ili kupata huduma za kibingwa na bingwa bobezi kutoka kwa madaktari bingwa wa Rais Samia.
Amesema kuwa huduma hizo zimesogezwa karibu na maeneo yao, hivyo ni jukumu la kila mwenye uhitaji wa matibabu kuchangamkia fursa hiyo, kwani inasaidia kupunguza gharama zisizo za msingi za kusafiri umbali mrefu kwenda hospitali za taifa, kanda, na mikoa.