Na Josea Sinkala, Mbeya.
Wananchi wa kitongoji cha Isyasya kijiji cha Mwala kata ya Ilembo Tarafa ya Isangati wilayani Mbeya, wamelalamikia kukosa huduma ya maji safi katika kitongoji chao ambacho kiko mbali kutoka makao makuu ya kijiji mpakani na Ngulilo wilaya ya Ileje mkoani Songwe.
Wananchi wameeleza hayo kwenye mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Mbeya vijijini Oran Manasse Njeza aliambatana na wataalam wa Halmashauri na mamlaka mbalimbali kwa ajili ya kueleza utekelezaji wa miradi na kusikiliza kero zao (wananchi).
Wamesema kitongoji chao kiko mbali na kijiji lakini ni kitongoji kikubwa ambacho walishawasilisha maombi ya kuwa kijiji kikipakana na wilaya ya Ileje ambapo hawana huduma ya maji safi huku barabara pia zikiwa sio rafiki na kumuomba mbunge kufuatilia utatuzi wa kero zao hasa ubovu wa barabara na ukosefu wa maji safi ikiwemo shuleni.
Akijibia changamoto hiyo kaimu meneja wa wakala wa maji vijijini (RUWASA) wilaya ya Mbeya Mhandisi Evetha Nzogela, amesema tayari wameshaombea fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi wa maji katika kijiji cha Mwala ambayo yatafika hadi kitongojini hapo na kumuomba mbunge kuendelea kushawishi upatikanaji wa fedha ili wafanikiwe kutekeleza mradi huo na kuwasaidia wananchi kwakuwa ni haki yao kupata huduma rafiki.
Kuhusu ubovu wa barabara Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) wilayani Mbeya Mhandisi Arcad Tesha, amesema barabara kubwa ambayo ni tegemeo kwa wananchi hao kutoka Ilembo Mwala hadi Isyasya na barabara nyingine ya Ilembo Shizuvi Isonso kwa ujumla zimeshaidhinishiwa fedha kiasi cha shilingi bilioni mbili na milioni mia sita kwa ajili ya ujenzi na sasa wapo kwenye hatua ya manunuzi (kutafuta mkandarasi) hivyo kuwaondoa hofu kuwa Serikali itatekeleza ahadi hiyo kwa kuwa tayari fedha zimeidhinishwa.
Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Oran Njeza, amewataka wananchi kuendelea kuiamini Serikali yao kwani anaendelea kuiomba fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali kama ambavyo baadhi imetekelezwa na kuweka historia ikiwemo usambazaji wa nishati ya umeme na miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ikiwemo katani humo na kudai ataendelea kuwawakilisha vizuri kwa kipindi chake kilichosalia.