Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) bara, Stephen Wasira, amesema kauli mbiu ya “No Reform, No Election” haina maana yoyote kwa sasa, akisisitiza kuwa muda wa kufanya mabadiliko ya kisheria umekwisha kutokana na uchaguzi mkuu kukaribia.
Akizungumza Januari 23, 2025, jijini Dodoma, Wasira ameeleza kuwa badala ya kushikilia kauli hiyo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanapaswa kushiriki uchaguzi na kuhakikisha wanakubaliana na maridhiano yaliyopo.
“Kauli ya ‘No Reform, No Election’ haina nafasi kwa sasa. Rais Samia Suluhu Hassan na CCM wameonesha utayari wa mazungumzo, na bunge linakaribia kuvunjwa, hivyo hakuna muda wa kufanya mabadiliko ya kisheria yanayohitaji muda mrefu,” amesema Wasira.
Ameongeza kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu, unaotarajiwa kuchagua Rais, Wabunge, na Madiwani, unapaswa kuwa nafasi ya vyama vyote kushindana kwa hoja badala ya kutafuta visingizio.
Wasira amewataka viongozi wa CHADEMA kutumia nafasi za mazungumzo zilizopo badala ya kusimamia misimamo isiyotekelezeka kwa wakati huu.
“Ni muhimu kushiriki uchaguzi na kuwa sehemu ya demokrasia badala ya kupoteza muda na kauli ambazo hazina tija kwa wananchi,” amesisitiza.