Latest Posts

WASIRA ALAANI SHAMBULIO DHIDI YA PADRI KITIMA “POLISI WAFANYE UCHUNGUZI WA KINA”

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amelaani tukio la kihalifu lililofanywa dhidi ya Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dkt. Charles Kitima, na kutaka uchunguzi wa kina ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, Wasira amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kushambuliwa kwa Padri Kitima akiwa katika ofisi za TEC, Kurasini, Dar es Salaam, akitoa pole na kuwataka polisi kuhakikisha haki inapatikana.

“Kama M/Mwenyekiti CCM (Bara), nimepokea kwa masikitiko taarifa ya tukio la kihalifu dhidi ya Pr. Dkt. Kitima katika ofisi za Baraza la Maaskofu. Natoa pole zangu na kulaani kitendo hiki. Polisi wafanye uchunguzi wa kina, kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua kali za kisheria,” ameandika Wasira.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Mei 1, 2025, majira ya saa nne na robo usiku, muda mfupi baada ya Padri Kitima kuhitimisha kikao cha viongozi wa dini.

“Baada ya kikao, Padri Kitima alielekea kwenye kantini ya baraza na kubaki hapo hadi saa nne na robo usiku, alipokwenda maliwatoni na ndipo alipojeruhiwa kichwani na watu wawili waliotumia kitu butu,” alisema Muliro.

Padri Kitima alikimbizwa Hospitali ya Aga Khan na kwa sasa anaendelea kupatiwa matibabu ambapo hali yake inaendelea vizuri.

Jeshi la Polisi linamshikilia Rauli Mahabi/Haraja, mkazi wa Kurasini, kwa mahojiano huku uchunguzi ukiendelea ili kubaini chanzo cha tukio hilo na kuhakikisha wote waliohusika wanakabiliwa na hatua kali za kisheria.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!