Latest Posts

WASIWASI WATANDA KWA KADA WA CHADEMA GEITA ANAYEDAIWA KUTEKWA KISHA KUKUTWA POLISI

Watanzania wamepewa rai ya kutofumbia macho vitendo vya utekaji na mauaji vinavyotajwa kuota mizizi hapa nchini siku za hivi karibuni badala yake wanapaswa kuchukua hatua kila mmoja anavyoona inafaa ikiwemo kupaza sauti ya kupiga vita vitendo hivyo vinavyokwenda kinyume na sheria na Katiba hasa katika kusimamia haki ya kutoa maoni na kuishi

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) mkoa wa Geita Justine Octavian alipofanya mahojiano kwa njia ya simu na Jambo TV Jumamosi Septemba 21.2024 kuhusiana na madai ya kutekwa na kisha kupatikana kwa kada na hamasa wa CHADEMA mkoani humo Khamis Omar Khamis, ambapo katika maelezo yake amebainisha kuwa kada huyo mkazi wa wilaya ya Chato anadaiwa kutekwa Septemba 07.2024 na kabla ya kupatikana usiku wa Septemba 19.2024

Octavian ameieleza Jambo TV kuwa licha ya kijana huyo kupatikana lakini kwa sasa wamejawa na wasiwasi kuhusiana na usalama wake kwa kuwa muhusika anadai kuwa kwa kipindi chote alichokuwa mateka alikuwa amefungwa kitambaa usoni na kamba mikononi kwa nyuma jambo ambalo lilikuwa linamuwia vigumu kutambua maeneo aliyokuwepo, na kwamba siku aliyopatikana alijikuta akidondoshwa kutoka ndani ya gari na baadaye kujikuta kwenye kituo cha Polisi

Amedai kuwa wasiwasi umekuwa mkubwa zaidi kwao kwani muhathirika anasema kipindi hicho cha mateka amekuwa akichomwa sindano ambazo haijafahamika mara moja ni za nini na alikuwa akichomwa kwa sababu zipi, jambo ambalo linapelekea kwa sasa ndugu, jamaa na marafiki waanze mchakato wa kumfikisha Hospitali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kina kuhusu afya yake

Jambo TV imezungumza na muhathirika wa tukio hilo Khamis Omar Khamis kupitia simu ya mama yake mzazi aitwaye Amina Daudi ambapo kwa sasa wanaishi Nyarugusu, Chato, mkoani Geita ambapo katika maelezo yake Khamis amesema hana kumbukumbu ya matukio yote yaliyokuwa yanatendeka kwa kipindi chote alichokuwa mateka lakini kwa kiasi kikubwa anakumbuka baadhi ya mazungumzo waliyokuwa wanaongea watekaji, ambapo mara nyingi alikuwa akiwasikia wakiongea na simu na mtu waliyekuwa wakimuita ‘mkuu’, na kwamba amekuwa pia akiwasikia wakisema ‘mkuu tumeshampata tayari, tunasubiri maelekezo yako’, lakini amesema watu hao endapo akikutananao anawafahamu kwa sura kwa kuwa aliwaona siku walipomteka.

Kuhusu mazingira ya kutekwa kwake Khamis amesema awali alikwenda kumtafuta rafiki yake aliyekuwa amechukua simu yake na kwamba katika kumtafuta rafiki yake aliongozana na Bodaboda (ambaye pia ni rafiki yake), na kwamba walipofika kwenye eneo alilokuwepo rafiki yake huyo walimuona kama mtu mwenye wasiwasi ndipo wakashuka kwenye pikipiki na kuanza kuongeanae lakini baada ya muda mfupi walivamiwa na watu ambao hawakuwafahamu ambao walikuwa ndani ya gari nyeupe iliyokuwa imepaki karibu yao, ndipo walipomkamata kwa nguvu kisha kumuingiza kwenye gari hiyo na baadaye kumfunga kitambaa usoni, kamba/ pingu mikononi kwa nyuma na kutokomea kusikojulikana

Ili kufahamu namna Khamis aliyopatikana, Jambo TV imezungumza kwa njia ya simu pia na Mzee Lucas Michael Ali (Maksai) ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAZECHA) mkoa wa Geita ambaye anayedaiwa kupigiwa simu ya kuelezwa kuhusu kupatikana kwa Khamis

Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo wa BAZECHA mkoa wa Geita anadai kuwa alipigiwa simu na Polisi Ijumaa ya Septemba 20.2024 kwenye majira ya kati ya saa 04 asubuhi na saa 06 mchana ambapo alielezwa kuwa afike kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Chato kumchukua ndugu yake kwani amepatiana, na kwamba pindi alipofika kituoni hapo alifika moja kwa moja kwenye ofisi ya Mkuu wa upelelezi wilaya ya Geita na kumkuta pia Khamis akiwa ofisini ameketi ofisini humo, ingawa hajafahamu kama ni mzima wa afya ingawa amemshuhudia akitembea sawasawa

Anasema alipouliza amefikaje kituoni hapo akajibiwa kuwa ameletwa na Polisi waliokuwa doria usiku wa kuamkia siku hiyo, hata hivyo aliruhusiwa kuondoka na Khamis huku wawili hao wakitakiwa kuripoti kituoni hapo kila baada ya siku nne (4), hivyo wanatarajiwa kuripoti kwa mara ya kwanza Jumatatu ya Septemba 23.2024

Jambo TV inaendelea kufuatilia kwa undani jambo hilo, ambapo kwa sasa tunaendeleza jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi mkoa (RPC) Geita ili atueleze namna Jeshi la Polisi mkoani humo linavyofahamu kuhusu undani wa tukio hilo lililogusa hisia za wengi ndani na nje ya mkoa wa Geita, kwa kuwa inadaiwa kuwa kabla ya kupatikana kwake awali ndugu, jamaa na marafiki walifanya jitihada za kupita kwenye vituo mbalimbali vya Polisi kumuulizia lakini walijibiwa kuwa hayupo na hajashikiliwa na Polisi kama ilivyokuwa ikidhaniwa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!