Latest Posts

WATAALAMU KUANZA KUCHUNGUZA UBORA WA MAJI ZIWA VICTORIA

Timu ya wataalamu kutoka nchi za Afrika Mashariki (Tanzania, Kenya na Uganda) zinazozungukwa na Ziwa Victoria wanatarajia kuanza kufanya utafiti wa kuchunguza na kubaini ubora wa maji hayo.

Akizungumza mara baada ya kufanya kikao kifupi kabla ya kuanza zoezi hilo la kukusanya sampuli za maji hayo, Naibu Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) Mhandisi, Coletha Ruhamya amesema uwepo wa aina mpya ya magugu maji Ziwa Victoria na shughuli za kibinadamu zinazofanyika kandokando ya ziwa hilo ni moja ya sababu zilizowafanya  kuja na utafiti huo.

“Sio kwamba tumeona kitu ila tunahisi kwamba kuna mambo ambayo siyo ya kawaida ukiangalia kwa jicho la kawaida muonekano wa ziwa lakini ukiangalia namna watu wanavyoongelea magugu maji pia hata ukiangalia shughuli za kibinadamu zinazofanyika kandokando ya ziwa Victoria, tunajua ukiona maji ni meupe au hayana rangi sio kwamba ni masafi ndio maana tukasema ngoja tufanye huu utafiti,” amesema.

Ameongeza kuwa “Madhumuni ya zoezi hili kwanza tunataka tujue ziwa hili limekaaje, tukifanya huu utafiti tukijua jinsi usafi ulivyo au uchafu unakotoka na kujua vitu vinavyofanyika katika bonde ili tuweze kutengeneza miradi ambayo itasaidia kupunguza huo uchafuzi,” amesema.

Akiunga mkono hoja hiyo Mkurugenzi wa Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Viktoria (LVBWB), Dk Renatus Shinhu amesema mara baada ya kufanya utafiti huo itawasaidia kuja na mbinu nzuri za kukabiliana na uchafuzi wa maji ziwa Victoria.

“Tunapopata takwimu za ubora wa maji tunapozichakata zinatusaidia kuja na miradi itakayotumika kuboresha na kuimarisha utunzaji wa vyanzo vyetu vya maji hasa Ziwa Victoria kwa sababu ukishajua ubora wako uko sehemu furani utajua wapi uimarishe,” amesema Dk Shinhu

Mshauri wa ufundi kutoka Shiriki la maendeleo la Ujerumani (GIZ), Omary Iddi Myanza ambao ndio wafadhili wa utafiti huo amesema wameamua kufadhili mradi huo ili kupata takwimu na taarifa zitakazosaidia jumuiya kutatua changamoto zinazolikumba ziwa hilo

“Tunafadhili zoezi hili kwa sababu takwimu na taarifa zitakazopatikana zitasaidia Jumuiya ya Afrika mashariki na bonde la ziwa Victoria kuweka mikakati thabiti ya kudhibiti mazingira ya ziwa hilo tumeona saizi kuna vitu vingi vinajitokeza suala la magugu maji na masuala ya samaki yote yanategemea ubora wa Ziwa Victoria,” amesema Myanza

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!