Latest Posts

WAZIRI MCHENGERWA AKANUSHA TAARIFA ZA VITUO BANDIA VYA UANDIKISHAJI KWA UCHAGUZI WA MITAA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa, amekanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusu uwepo wa vituo bandia vya kuandikisha wapigakura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Akizungumza na vyombo vya habari tarehe 15 Oktoba 2024, jijini Mwanza, Mchengerwa alisema kuwa taarifa hizo sio za kweli, na kufafanua kuwa uandikishaji unafanyika katika vituo halali 80,812 kote nchini.

Mchengerwa ameeleza kuwa, kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 796 na 797, jumla ya mitaa na vitongoji vinavyoshiriki uchaguzi ni 68,543, lakini idadi ya vituo ni 80,812 kutokana na baadhi ya mitaa au vitongoji kuwa na vituo zaidi ya kimoja.

“Lengo la kuwa na vituo hivi ni kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na kupata haki yao ya msingi ya kuchagua na kuchaguliwa,” amesisitiza Mchengerwa.

Waziri huyo ameeleza zaidi kuwa vituo vya ziada vinaongezwa katika baadhi ya maeneo kutokana na wingi wa watu au jiografia ngumu ya maeneo husika, kama vile misitu, maeneo ya wafugaji, wakulima, wachimbaji migodini, au wananchi wanaoishi mbali na vituo vya uandikishaji.

Mchengerwa ameendelea kusema kuwa kutowapa wananchi fursa ya kuwa na kituo karibu ni kuwanyima haki yao ya kikatiba. Ameeleza kuwa, kwa mujibu wa kanuni, vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi vinapaswa kukubaliana na wasimamizi wa uchaguzi ili kuamua ni wapi kituo cha kuandikisha na kupiga kura kiwekwe, kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata haki yao ya kikatiba bila vikwazo.

Aidha, Waziri Mchengerwa amewataka wadau wa vyama vya siasa na wasimamizi wa uchaguzi kushirikiana kikamilifu kuhakikisha vituo vya uandikishaji vinapatikana katika maeneo yote yanayohitaji, kwa lengo la kufanikisha zoezi la uandikishaji kwa wananchi wote pasipo vikwazo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!