Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, ametoa mwezi mmoja kwa Kituo cha Afya Segese kuanza kutoa huduma baada ya kukamilika kwa ujenzi na kuwa na baadhi ya vifaa tangu mwaka 2023. Hali hii inasababisha wananchi kukosa huduma muhimu za afya ya uzazi na upasuaji.
Ndejembi alitoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Msalala, wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
“Ninamuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala kuhakikisha kwamba ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa, kituo hiki kinaanza kutoa huduma kwa wananchi. Lengo la Serikali ni kusogeza huduma karibu na wananchi na siyo kuwaacha watembee umbali mrefu,” alisema Ndejembi.

Aidha, Waziri Ndejembi aliupongeza mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Ntobo, ambao umekamilishwa kwa gharama ya Sh. Milioni 170.8, badala ya Sh. Milioni 182, na hivyo kubakiza chenji ya Sh Milioni 11.1.
Katika kukagua ujenzi wa shule hiyo, Ndejembi alisifu juhudi na uwajibikaji wa kamati ya ujenzi kwa kutumia fedha kwa ufanisi.
“Mara nyingi tunapokea taarifa za miradi ya maendeleo ambapo fedha huisha kabla ya mradi kukamilika, lakini hapa Ntobo miradi imekamilika kwa kiwango cha juu na chenji imebaki. Haya ndio matumizi bora ya fedha za umma ambayo Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anatuelekeza tuyafuate,” alisisitiza.

Katika ziara hiyo, Waziri Ndejembi pia alizungumza na wananchi wa Msalala na kuwakumbusha mafanikio makubwa yaliyofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika sekta mbalimbali, ikiwemo Afya, Elimu, Maji, na Miundombinu katika Halmashauri hiyo.