Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, amesema kuwa Serikali imekusudia kuimarisha ushirikiano na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ili kukuza dhana ya utawala bora kwa maendeleo ya taifa.
Akizungumza baada ya kutembelea viongozi wa TLS jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Simbachawene amesema kuwa TLS ina nafasi kubwa katika kusimamia utawala wa sheria, ambao ni msingi wa utawala bora.

“Nimekuja kuwatembelea kwa sababu niligundua kuwa kila ninapotekeleza majukumu yangu katika kusimamia utawala bora, TLS ina nafasi muhimu sana,” amesema Simbachawene.
Amefafanua kuwa kwa mujibu wa Sheria ya TLS SURA 307, chama hicho ni chombo cha umma kilichoanzishwa kwa mujibu wa sheria ya Bunge, hivyo ushirikiano wake na serikali unapaswa kuwa wa wazi na sio kuonekana kama harakati zisizo rasmi.
Ameongeza kuwa TLS ina historia ndefu, na ni chombo kilichokuwepo kabla ya uhuru lakini mpaka wakati huu kinafanya kazi nzuri na kinashirikiana na serikali katika maeneo mbalimbali, hivyo kutokana na ushirikiano uliopo na Serikali, akiwa ndiye Waziri mwenye dhamana ya utawala bora akaona asikae nyuma badala yake awatembelee ili apate cha kujifunza katika utekelezaji wa majukumu yake.

Amesema yako maeneo mapana ya kushirikiana ili kujenga utawala bora na utawala wa Sheria ambao utasaidia upatikanaji wa haki, kukua kwa amani na utulivu kwa maendeleo ya nchi ya Tanzania.
Katika kikao hicho, Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi, ameeleza kuwa chama hicho kinapendekeza kuhusishwa katika maamuzi ya kitaifa yanayohusiana na sheria, hususan katika mikataba mikubwa ya kitaifa.
“TLS ina wataalamu waliobobea katika masuala ya sheria, na ushirikiano na serikali utakuwa na manufaa makubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla,” amesema Mwabukusi.

Aidha, Wakili Mwandamizi Mpale Mpoki ameshauri serikali kuhakikisha utekelezaji wa maamuzi ya Mahakama ambayo yamechukua muda mrefu bila utekelezaji. Ametaja miongoni mwa kesi hizo kuwa ni kesi ya Rebeca Gyumi, kesi ya Mtobesya, na kesi ya Kabourou ya vyama vingi.