Watu wenye ulemavu nchini wameungana kwa dhati kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ya kuleta maendeleo jumuishi nchini, kwa kumchangia Shilingi milioni moja kwa ajili ya kugharamia fomu ya kugombea nafasi ya Urais kwa mwaka 2025.
Wamesema kuwa mchango huo ni alama ya shukrani kwa kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, ikiwemo maboresho katika sekta ya afya, elimu, miundombinu, na ushirikishwaji wa watu wenye mahitaji maalum katika mipango ya taifa.
Katika tukio jingine, wakati Serikali ikijiandaa kuanza utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, wadau wameitaka Serikali kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu hawaachwi nyuma. Wito huo umetolewa kwenye mkutano wa kitaifa wa mashauriano kuhusu mgao wa asilimia 30 ya Samia kupitia mfumo wa NeST kwa watu wenye mahitaji maalum, uliofanyika jijini Dodoma hivi karibuni.
Muasisi wa Ikupa Trust Fund, Stella Ikupa, amesema licha ya hatua zilizopigwa na Serikali, bado watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto kama vile ukosefu wa vifaa saidizi, miundombinu isiyofikika, na uhaba wa wahudumu wa afya waliobobea katika kuhudumia watu wenye ulemavu.
“Mpango wa bima ya afya kwa wote hauwezi kufanikiwa ikiwa hautazingatia mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu,” amesisitiza Ikupa.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, ameeleza kuwa Serikali imeendelea kutoa mafuta maalum kwa watu wenye ualbino ili kuwakinga na saratani ya ngozi. Pia ameahidi kuimarisha usimamizi wa sera zinazolenga kuwawezesha watu wenye ulemavu kijamii na kiuchumi.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa PPRA, Bi. Winfrida Samba, amefafanua kuwa mfumo wa NeST umewezesha watu 1,335 wenye ulemavu kusajiliwa kama wazabuni wa Serikali, hatua inayoongeza uwazi na ushiriki wao katika manunuzi ya umma.
Wadau wameitaka Serikali na mashirika ya kiraia kushirikiana kwa karibu kuhakikisha kuwa utekelezaji wa sera ya Bima ya Afya kwa Wote unakuwa jumuishi, unaozingatia mahitaji ya makundi yote, bila ubaguzi.