Kampuni ya Maestro Africa Solutions Ltd, kwa kushirikiana na Peak Performance Company Ltd na Rehoboth Organization na The Ark Africa wameandaa Maonesho Maalum ya Baby Market yatakayofanyika tarehe 28 mwezi huu katika Viwanja vya Sayansi, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Maestro Africa Solution, Amaris Mwako wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa kampeni ya iCARE Watoto inayolenga kuhamasisha jamii kuwajali watoto.
Amesema tukio hilo maalum limeandaliwa kwa lengo la kuwa ‘One Stop Center’ kwa kila kitu kinachomhusu mtoto, kuanzia bidhaa, huduma hadi taarifa muhimu kutoka kwa kampuni zinazohudumia watoto, taasisi zinazojihusisha na ustawi wa mtoto na shule za awali na msingi.


Amesema tukio hilo linawalenga watoa huduma za afya na lishe kwa watoto, vifaa vya watoto, mavazi, michezo, elimu na zaidi!
“Haya siyo maonesho ya kawaida tu. Ni jukwaa la watoto kuonesha vipawa vyao (talent showcase) na watoto kuuza bidhaa walizotengeneza wenyewe na wa watoto kushiriki kama mawakala wa masoko (PR) wa miradi ya wazazi wao,” amesema na kuongeza,
“Tunaamini ni muhimu kupanda mbegu njema mapema kwa kuwaandaa watoto kuwa warithi wa miradi, biashara na maono ya familia zao. Tumeona mara nyingi mipango mizuri ya wazazi hufa kwa kukosa maandalizi ya kizazi kijacho. Sisi tunasema: Sio lazima kila kizazi kianze upya – tunaweza kujenga vizazi vinavyoendeleza vilivyoanzishwa”.
Amesema wamealika benki na taasisi mbalimbali kuonesha huduma zao kwa familia, na mashirika ya maendeleo ya watoto kuonesha programu zao, “na tunapendekeza mje na watoto mliowasaidia, ambao wanaweza kuwa mabalozi wenu wadogo”.
Amesema Kampeni ya iCARE Children na maonesho hayo pia yanahamasisha kampeni ya iCARE watoto-Wote Tunahusika inayosisitiza kuwa kila mtu ana jukumu la kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama, yenye upendo na nafasi ya kustawi.
Amesema siku hiyo kutakuwa na michezo mbalimbali kwa watoto, maonesho ya vipaji, huduma za afya na lishe na wadau wa elimu mbadala miongoni mwa mambo mengine.