Na Amani Hamisi Mjege.
Â
Kampuni mbili kubwa, Adani Group ya India na Gridworks Development Partners LLP ya Uingereza, zimeonesha nia ya kuwekeza katika mradi wa kusafirisha umeme nchini Tanzania kupitia mfumo wa ubia. Mradi huo unalenga kujenga njia za kusafirisha umeme wa juu kwa lengo la kuboresha miundombinu ya nishati nchini Tanzania.
Â
Akizungumza kwa njia ya simu na Jambo TV, David Kafulila, Kamishna wa Ubia wa Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), amefafanua kuwa utaratibu huo unajulikana kama “expression of interests,”ambapo wawekezaji wanaweza kueleza nia yao ya kuwekeza kwenye miradi kwa kushirikiana na serikali.
Â
“Kampuni (Wawekezaji) mbili ambazo zimeomba kufanya mradi wa kusafirisha umeme kwa utaratibu wa ubia, inaitwa expression of interests yaani kwamba inaruhusu mwekezaji kueleza nia yake ya kuwekeza kwenye mradi fulani katika utaratibu wa ubia na serikali” ameeleza Kafulila.
Â
Kafulila ameeleza zaidi kuwa sheria za ubia nchini Tanzania zinaruhusu kampuni kuwasilisha maombi yao kwa hatua za awali, na serikali inaweza kuamua kuitangaza miradi hiyo kwa kampuni zingine kushindana ili kuhakikisha uwazi na ufanisi. Hivi sasa, Adani na Gridworks ndio kampuni mbili zilizowasilisha maombi ya kuwekeza katika mradi huo wa kusafirisha umeme.
Â
Ameongeza kuwa zipo njia nne zinazotumika kuingia kwenye ubia wa umma na binafsi nchini Tanzania. Njia hizo ni pamoja na serikali kutangaza mradi na kuruhusu ushindani (solicited), mwekezaji kuomba kuandaa mradi (unsolicited), serikali kutafuta mwekezaji wa moja kwa moja wa haraka hasa baada ya kuwa tayari imeandaa mradi (direct negotiation), na ya utaratibu maalum (special arrangement). Katika kesi ya Adani na Gridworks, wameomba kuwekeza kupitia njia ya kusudio la mwekezaji (unsolicited).
Â
Kafulila amesisitiza kuwa maombi yaliyotolewa na Adani na Gridworks ni hatua ya awali, na michakato ya kuchunguza kama kampuni hizo zina sifa stahiki itaendelea. Serikali kupitia TANESCO itazingatia mahitaji ya mradi huo na kuamua kama kutangaza zabuni kwa kampuni zingine au kuendelea na kati ya waombaji wa sasa.
Â
“Adani ameleta kusudio awekeze, ni hatua ya awali ya kueleza kusudio, na siyo Adani peke yake ambayo imeomba iwekeze, sasa baadaye kwa mujibu wa sheria TANESCO sasa inaweza ikaamua kutangaza na kampuni zote ambazo zinahitaji zikashindana kutegemea mahitaji yake kwa wakati huo. Sasa hiyo iliyofanyika ya Adani na Kampuni nyingine ya Uingereza ya Gridworks Development Partners LLP, ni kampuni mbili ambazo zimeomba kuwekeza, na sheria inawaruhusu kuomba. Sasa ukiomba, ndiyo michakato inaanza ya kama una sifa au hauna sifa”, ameeleza Kafulila.
Â
Adani Group, kampuni inayoongozwa na bilionea Gautam Adani, imekuwa ikiongeza uwepo wake katika ukanda wa Afrika Mashariki, huku Tanzania ikiwa sehemu ya mikakati yao ya kuimarisha miundombinu ya nishati kupitia mradi unaotajwa kuwa na thamani ya takriban dola milioni 900. Tanzania pia iko kwenye mazungumzo na Gridworks Development Partners kuhusu mradi wa dola milioni 300.
Â
Kwa upande wake, Tanzania imeweka kipaumbele katika kuboresha miundombinu ya nishati ili kukidhi mahitaji ya umeme yanayoendelea kuongezeka, hatua inayosaidiwa na miradi kama hii ya ubia. Ushirikiano huu pia ni muhimu kwa kuboresha mfumo wa usafirishaji wa umeme wa juu nchini.