News, Njombe.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Njombe kimepiga marufuku makada wake wenye uwezo na nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo udiwani na ubunge kutoa misaada, michango na zawadi bila kuwepo taarifa rasmi za vikao vya ngazi husika huku akiwataka wadau wanaotoa michango kuhakikisha inapita kwa katibu na uongozi ukiwa unafahamu.
Agizo hilo limetolewa na Katibu wa Siasa na Uenezi mkoa wa Njombe Josaya Luoga wakati akizungumza na vyombo vya habari ambapo pia amesema halmashauri kuu ya chama hicho mkoa wa Njombe imeelekeza kamati za maadili kwenye majimbo na wilaya zote kuhakikisha zinapata taarifa za kutosha juu ya wanachama na viongozi wanaofanya kazi ya ukuwadi kwa wanachama wanaotamani kuwa viongozi 2025.
“Mambo yanayokatazwa ni kutoa michango, misaada na zawadi pasipokuwa na taarifa wala vikao rasmi vilivyoidhinishwa na vikao vya ngazi husika na michango hiyo kama mdau anatoa ipite kwa katibu na uongozi ufahamu kwamba huyo ni mdau hana madhara kwenye utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2020-2025 “, amesema Luoga.
Aidha Luoga amesema CCM imepiga marufuku viongozi kukusanya michango kwa watu wanaodhani wanawatengeneza kuwa wagombea wa ubunge na udiwani huku akibainisha kuwa limeibuka wimbi la vijana ambao kwa makusudi wanawakaribisha wagombea kinyume na utaratibu wa Chama badala ya kuwasaidia viongozi waliopo madarakani kuhakikisha wanatekeleza Ilani ili kuwa na majibu ya kutosha kwa wananchi unapofika wakati wa uchaguzi.