Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera, amemuagiza kamanda wa jeshi la nchi hiyo kujiandaa kuondoa wanajeshi wa Malawi kutoka Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwa mujibu wa taarifa ya televisheni ya serikali.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa uamuzi huo unalenga “kuheshimu tangazo la kusitisha mapigano”, ingawa kusitishwa kwa mapigano kulivunjika baada ya waasi wa M23 kushambulia mji wa Nyabibwe, Kivu Kusini.
Rais Chakwera alikuwa chini ya shinikizo la kisiasa la kuondoa wanajeshi wake baada ya wanajeshi watatu wa Malawi kuuawa katika mashambulizi ya M23 mjini Goma.
Wanajeshi wa Malawi walikuwa sehemu ya vikosi vya kulinda amani vya SADC vilivyotumwa kusaidia mamlaka ya DRC kudhibiti makundi yenye silaha.
Baada ya M23 kuteka Goma, kundi hilo sasa linajaribu kuingia Kivu Kusini, wakilenga mji wa Bukavu. Tayari, waasi hao wameanza kuteua viongozi wao, wakiwemo magavana wa Kivu Kaskazini.
Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa takriban watu 3,000 waliuawa katika mapigano ya M23 wakati wa kuuteka Goma, huku kukiwa na hofu ya kuenea kwa magonjwa kama Mpox na kipindupindu nje ya jiji hilo.