Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) unatarajiwa kuondoa changamoto ya ucheleweshaji wa malipo kwa wazabuni mara baada ya kuunganishwa kikamilifu na mifumo ya malipo na bajeti ya Serikali, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeelezwa.
Wasilisho hilo lilitolewa na Public Procurement Regulatory Authority (PPRA) mbele ya Kamati hiyo katika Ukumbi wa Bunge, Dodoma, likihusu maendeleo ya usimamizi wa sekta ya ununuzi wa umma nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba, amesema kuwa mfumo wa NeST tayari una moduli sita kuu ambazo ni Usajili, Uchakataji wa Zabuni, Usimamizi wa Mikataba, Upokeaji wa Malalamiko, Mnada wa Kielektroniki pamoja na Malipo ya Kielektroniki (e-payment).

Ameeleza kuwa moduli ya malipo imeunganishwa na mifumo ya Serikali ya MUSE na EMRS, huku hatua za mwisho za kuunganisha mfumo huo na mifumo ya bajeti zikiendelea kukamilishwa.
Amebainisha kuwa mara baada ya kupata kibali cha Serikali, taasisi haitaruhusiwa kuanzisha mchakato wa ununuzi bila kuwa na kifungu cha bajeti kilichotengwa na kuzuiwa kwenye Mfumo wa NeST tangu mwanzo wa mchakato.
Hatua hiyo inalenga kuondoa tatizo la baadhi ya watumishi kuanzisha zabuni bila uhakika wa fedha au kubadili matumizi ya vifungu vya bajeti katikati ya mchakato, hali inayosababisha ucheleweshaji wa malipo kwa wazabuni.

Simba amesisitiza kuwa ucheleweshaji huo hauwaumizi tu wazabuni bali pia unaiongezea Serikali gharama zisizo za lazima, kwani wazabuni hulazimika kuongeza riba (interest) kwenye madai yao wanapocheleweshewa malipo.
Aidha, ameeleza kuwa kuanzia mwezi Machi, NeST utaanza kutuma taarifa za tahadhari (red flag notifications) kwa zabuni zitakazobainika kuwa na viashiria vya ukiukwaji wa taratibu,mfumo huo utawezesha PPRA kuingilia kati mapema kabla ya mchakato kukamilika, badala ya kusubiri ukaguzi wa baadae.
Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Khalfan Aeshi, amepongeza PPRA kwa maboresho hayo na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu fursa za ununuzi wa umma, hususan utekelezaji wa asilimia 30 ya zabuni zinazotengwa kwa makundi maalum wakiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Profesa Leonada Mwagike, aliishukuru Kamati kwa ushauri na maelekezo yaliyotolewa, akiahidi kuwa Mamlaka hiyo itaendelea kuimarisha usimamizi na uwazi katika sekta ya ununuzi wa umma nchini kupitia Mfumo wa NeST.
