Latest Posts

UZALISHAJI WA SUKARI NYEUPE MKULAZI KUPUNGUZA GHARAMA ZA UAGIZAJI NJE

Mawaziri wawili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo, na Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo wametembelea Kiwanda cha Sukari Mkulazi mkoani Morogoro na kuagiza kiwanda hicho kuendelea kuzalisha sukari nyeupe ya viwandani ili kupunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje ya nchi.

Wakizungumza na menejimenti ya kiwanda hicho baada ya kupokea taarifa ya uzalishaji, mawaziri hao walieleza kuridhishwa na uwekezaji na usimamizi wa kiwanda hicho, wakisisitiza umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa sukari nyeupe ya viwandani ambayo Tanzania kwa sasa inaagiza kwa asilimia 100 kutoka nje.

Prof. Kitila alisema kwa sasa nchi inaagiza takribani tani 300,000 za sukari ya viwandani kila mwaka, hali inayosababisha matumizi makubwa ya fedha za kigeni.

“Kuanzishwa kwa uzalishaji wa sukari nyeupe ya viwandani hapa Mkulazi ni hatua kubwa katika kupunguza utegemezi huo. Lengo la Serikali ni kuona ifikapo mwaka 2026/2027 hadi 2027/2028 Tanzania inajitegemea kwa asilimia 100 katika uzalishaji wa sukari na ziada kuuzwa nje ya nchi,” amesema.

Ameongeza kuwa soko la sukari barani Afrika linakadiriwa kuwa na mahitaji ya zaidi ya tani milioni 12, hivyo Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika kiuchumi endapo uzalishaji utaongezeka.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo amesema uamuzi wa Mkulazi kuanza kuzalisha sukari nyeupe ya viwandani ni hatua muhimu katika kuimarisha sekta ya viwanda na kilimo.

Ametoa wito kwa wawekezaji, wakiwemo taasisi za hifadhi ya jamii kama NSSF, kuendelea kuwekeza katika viwanda vya sukari kutokana na fursa kubwa iliyopo ya mahitaji ya bidhaa hiyo ndani na nje ya nchi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amesema kiwanda cha Mkulazi ni miongoni mwa miradi muhimu inayochochea ukuaji wa uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.

Amepongeza menejimenti ya kiwanda hicho kwa utekelezaji mzuri wa mipango yao inayosaidia kupunguza tatizo la uhaba wa sukari nchini.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi, Selestine Some, amesema Mkulazi ndicho kiwanda pekee nchini kinachozalisha sukari nyeupe ya viwandani kwa sasa, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho.

Alisema baada ya kufanya majaribio ya uzalishaji katika msimu huu, msimu ujao kiwanda kitaongeza uzalishaji ili kupunguza kwa kiasi kikubwa uagizaji wa sukari ya viwandani kutoka nje.

Some aliongeza kuwa kiwanda kinatoa fursa kwa wakulima wa nje kuuza miwa kama malighafi. Kwa mwaka huu, wakulima wanatarajiwa kulima hekta 1,717, ambapo hadi sasa hekta 1,384 tayari zimelimwa, na wana matumaini ya kufikia lengo hilo msimu ujao.

Aidha, amesema ubora wa sukari inayozalishwa umeifanya kupendwa na walaji, huku akisisitiza kuwa kiwanda pia kimefanikiwa kuzalisha wataalamu wazawa watakaosimamia uzalishaji wa sukari nyeupe ya viwandani kwa ufanisi.

Kwa mafanikio hayo, Mkulazi inaendelea kuwa nguzo muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea kujitegemea kwa uzalishaji wa sukari na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!