Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla amezindua utaratibu wa usikilizaji kero na uwajibikaji kwa Watendaji wa Mitaa na Kata, akitangaza kuwa upimaji wa Viongozi hao katika utendaji utatokana na namna walivyotatua kero za wananchi katika maeneo yao.
Mhe. Makalla amezindua utaratibu huo leo Ijumaa Februari 27, 2026 alipokutana na Viongozi na Watendajj wa Halmashauri za Wilaya za Arumeru na Arusha pamoja na Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Wilaya za Mkoa wa Arusha, akisema asilimia kubwa ya kero zipo kwenye sekta ya ardhi katika ngazi ya Vijiji na Kata.

Katika maelekezo yake, Mhe. Makalla ameagiza kila Halmashauri kuwa na dawati la kusikiliza na kutatua kero za wananchi na kila Afisa ardhi kutenga siku moja kwa kila wiki kwaajili ya kushughulikia kero za wananchi katika maeneo yao.
Aidha Mhe. Makalla amebainisha kuwa Ofisi yake na Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Arusha wataendesha Kliniki maalumu za usikilizaji na utatuzi wa kero za wananchi, akiwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuimarisha na kuyajengea uwezo Mabaraza ya ardhi kupitia mafunzo na semina mbalimbali pamoja na kusisitiza Mabaraza hayo kutenda haki katika kuwahudumia wananchi.
