Mahakama ya Rufani ya Tanzania imetupilia mbali shauri la marejeo na 720316/2026 lililofunguliwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini(DPP) dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) Tundu Lissu ambalo lilitaka kupitiwa mwenendo na uamuzi wa Februari 24, 2026 katika kesi ya uhaini iliyopo Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.
Maombi hayo yalifunguliwa baada ya uamuzi mdogo kutolewa na Mahakama Kuu kukataa kuongezwa kwa ushahidi wa ziada wa ACP Amini Mahamba ambaye alikuwa Mpelelezi Mkuu wa matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025.
Uamuzi huo wa Rufani uliotolewa Julai 30, 2026 na Majaji wa Rufani Mwarija, Muruke na Khamis umeeleza kuwa mahakama ilikuwa sahihi katika uamuzi huo kwani kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai(CPA) kinaeleza juu ya ushahidi wa shahidi ambaye ushahidi wake haukusomwa kabisa katika Mahakama ya Ukabidhi (Commital Court) na sio ushahidi mpya wa shahidi ambaye ushahidi wake ulisomwa katika mahakama hiyo.
“Katika mazingira hayo, tunakubaliana na mahakama ya awali kwamba Kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kinamhusu shahidi ambaye hakutajwa wala ushahidi wake kusomwa kwa mshtakiwa wakati wa mwenendo wa awali wa kupeleka shauri Mahakama Kuu (committal proceedings).” umeeleza uamuzi
Uamuzi huo umeongeza “Kwa kuzingatia sababu zilizotangulia, tunaona kuwa notisi hiyo ilikuwa imewasilishwa kwa msingi usio sahihi wa kisheria (misconceived), na hivyo mahakama ya awali ilikuwa sahihi na ilijielekeza ipasavyo kuifuta (strike out).”
Ikumbukwe Februari 22, 2026 upande wa Jamhuri uliwasilisha mahakamani notisi ya ushahidi wa ziada wa ACP Mahamba juu ya ripoti ya matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi ambapo Lissu alipinga vikali kupokelewa kwa notisi hiyo akieleza ni kinyume na sheria hoja ambayo Mahakama iliikubali.
Aidha uamuzi huo umeyakataa maombi ya Lissu juu ya kutaka kulipwa fidia na DPP kwa kile alichoeleza kuwa ni kusababishiwa usumbufu kwa siku 139 huku ikielezwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa uamuzi huo kwa sasa haliyakuwa kesi bado haijafika mwisho.