Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limeweka wazi kuwa lengo kuu la kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kutoa mtazamo wao kuhusu hali ya kisiasa nchini na kushauri njia bora ya kuiponya nchi kufuatia matukio ya Uchaguzi Mkuu uliopita.
Akizungumza na waandishi wa habari leo kufuatia kikao hicho kilichofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, Agosti 10, 2026, Katibu Mkuu wa TEC, Padre Dkt. Charles Kitima, amebainisha kuwa mkutano huo ulitokana na ombi la maaskofu wenyewe waliotaka kumshirikisha Rais maoni yao.
Padre Kitima ameeleza kuwa maaskofu wamewasilisha andiko rasmi lenye kurasa nne ambalo linasisitiza umuhimu wa kusimamia ukweli na msamaha ili kurejesha utulivu wa kweli nchini.
“Kutokana pia na kwamba waliweka eh bayana kwamba ili tutoke katika hali hii inabidi kwenda katika kusimamia ukweli na vile vile kutakana msamaha, kusameheana na hata kuponya nchi. Kwa hiyo kwa kiingereza tunasema ‘to admit the truth then reconciliation healing the nation’,” amesema Padre Kitima.
Padre Kitima amewataka Watanzania kuwa na imani na ujumbe uliowasilishwa na maaskofu na kuwa na utulivu wakati serikali ikielekea katika kutatua mkwamo wa kisiasa uliopo nchini.