Kesi ya uhaini namba 19605/2025 inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antiphas Lissu, imeendelea leo mchana katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam. Shauri hilo lilirejea saa nane na dakika 50 mchana kufuatia mapumziko mafupi, ambapo mshitakiwa Tundu Lissu, akisimama kama shahidi wa kwanza wa utetezi kwenye kesi yake, aliendelea kutoa ushahidi wake mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru.
Katika utetezi wake vya leo Agosti 24, 2026, Lissu ameeleza siri ya mazungumzo yake na Rais Samia Suluhu Hassan akiwa uhamishoni Ubelgiji, mazingira yaliyosababisha kufa kwa “maridhiano” kati ya CHADEMA na CCM, chimbuko la kampeni ya “No Reforms No Election”, na jinsi alivyoshtakiwa kwa uhaini kwa kutumia maneno aliyodai kuwa yalichukuliwa nje ya muktadha.
Akianza ushahidi wake baada ya mapumziko, Lissu alionya kuwa masuala ya uchaguzi na katiba yasipowekwa sawasawa na kutatuliwa kwa amani, huwa yanaleta maafa makubwa na umwagaji wa damu. Alitolea mfano wa kihistoria wa Zanzibar, akieleza kuwa Muungano wa Tanzania ulitokana na Mapinduzi ya Zanzibar yaliyosababishwa na uonevu na dhuluma za uchaguzi, kama ilivyochambuliwa na Ripoti ya Tume ya Nyalali ya mwaka 1992.
Lissu amedai kuwa baada ya kufariki kwa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, John Pombe Magufuli, na kuingia madarakani kwa Rais Samia Suluhu Hassan, yeye (Lissu) alikuwa bado anaishi uhamishoni nchini Ubelgiji. Mnamo tarehe 17 Februari 2022, wakati wa Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya (AU-EU Summit) huko Ulaya, Rais Samia alimtumia ujumbe akieleza kuwa anataka waonane. Wakati huo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alikuwa bado gerezani akikabiliwa na tuhuma za kigaidi.
Katika mazungumzo yao, Rais Samia alimweleza Lissu kuwa alikuwa anatamani “kusafisha na kusawazisha matatizo yote yaliyoachwa na mtangulizi wake”. Lissu ameeleza kuwa alimjibu Rais Samia kuwa kama kweli ana nia hiyo, basi jambo la kwanza la kufanya ni kumtoa Mwenyekiti Mbowe gerezani, na kisha kuanzisha mazungumzo ya kitaifa kuhusu Katiba Mpya, mfumo huru wa uchaguzi, na kupata Tume Huru ya Uchaguzi.
Aidha, Lissu alimtaka Rais Samia kutoa tamko rasmi la kuwahakikishia usalama viongozi waliokimbia nchi akiwamo yeye mwenyewe, Godbless Lema, na Ezekiah Wenje ili waweze kurejea nyumbani salama. Baadaye, Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo alitoa tamko hilo, viongozi waliokuwa uhamishoni wakarejea nchini.
Kufuatia kurejea kwa viongozi hao na kuachiwa kwa Mbowe, mazungumzo rasmi ya kisiasa yaliyojulikana kama “Maridhiano” yalianza, yakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM kwa wakati huo, Abdulrahman Kinana, na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHADEMA kwa wakati huo.
Lissu ameeleza kuwa katika vikao hivyo, CHADEMA iliwasilisha mapendekezo ya kina na ya maandishi yaliyotaka mabadiliko ya kikatiba, muundo huru wa Tume ya Uchaguzi, na ratiba ya mabadiliko ambayo ingewezesha nchi kupata Katiba Mpya ifikapo mwaka 2024. Hata hivyo, CCM ilionesha kukosa utayari kwa kujibu mapendekezo hayo kwa mdomo tu na kukataa kutoa majibu ya maandishi kwa karibu mwaka mzima.
Aliporejea nchini kutoka uhamishoni, Lissu amesema aliwaambia viongozi wenzake wa CHADEMA kuwa “maneno maneno hayawezi kutufikisha kokote” na kusisitiza kuwa CCM lazima waandike rasmi kama wanakubali au kukataa mapendekezo yao. Baadaye, CCM walitoa majibu ya maandishi wakiyakataa mapendekezo yote ya CHADEMA.
Kufuatia hatua hiyo, Kamati Kuu ya CHADEMA ilifanya kikao na kuazimia rasmi kuwa “habari ya maridhiano ife” kwa kuwa ilionekana kuwa ni mtego wa kupoteza muda. Chama kiliamua kuirudisha kampeni ya kudai Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi moja kwa moja kwa wananchi ili iwe kampeni ya umma. Hata hivyo, mara baada ya joto la kisiasa kuanza kupanda nchini, wanachama na viongozi wa CHADEMA walianza kukabiliwa na mauaji, utekaji nyara, na kufunguliwa kesi mbalimbali.
Lissu ameendelea kujitetea kuwa uamuzi wa CHADEMA wa kudai mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi ulithibitishwa zaidi wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Novemba 2024. Uchaguzi huo ulisimamiwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI (sasa ikiwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu), ambayo kisheria ipo chini ya usimamizi wa Rais na wasimamizi wake ni wateule wa Rais.
Kwa mujibu wa Lissu, katika uchaguzi huo, wagombea karibu wote wa vyama vya upinzani walienguliwa kiholela ili kubakiza wagombea wa CCM pekee, huku baadhi ya wagombea wa upinzani kupoteza maisha. Amesema hali hiyo ilikivuruga chama na kuonesha kuwa mfumo uliopo hauwezi kuruhusu uchaguzi wa haki.
Mnamo tarehe 3 Oktoba 2025, Kamati Kuu ya CHADEMA ilifanya kikao cha dharura na kuja na azimio la kampeni ya “No Reforms No Election” (Hakuna Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi). Amesema kaulimbiu hiyo ilitangazwa rasmi hadharani tarehe 10 Desemba 2024 chini ya uongozi wa Freeman Mbowe wakati huo. Tarehe 20 Januari 2025, Kamati Kuu ilipeleka mapendekezo hayo kwa Baraza Kuu la chama ili iwe ajenda na sera rasmi, na tarehe 21 Januari 2025, Mkutano Mkuu wa CHADEMA ulipitisha msimamo huo chini ya uenyekiti wa Mbowe kabla ya Lissu kuchaguliwa.
Siku iliyofuata, tarehe 22 Januari 2025, Lissu alichaguliwa kuwa Mwenyekiti Mpya wa CHADEMA Taifa na kurithi msimamo huo ambao ulikwishakuwa sera rasmi ya chama. Kama Mwenyekiti mteule, alimteua John Mnyika kuwa Katibu Mkuu na Amani Golugwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara ili kutengeneza mkakati wa utekelezaji wa “No Reforms No Election”.
Lissu amesisitiza kuwa mkakati huo ulipanga kutumia njia za kidemokrasia na za kisheria kama maandamano ya amani na kususa, na haukuhusisha hata kidogo kufanya fujo, kuchoma nyumba au magari, au kupanga kuipindua serikali kwa uhaini. Amesema kama chama walijitahidi kueneza msimamo huo kwa kuonana na taasisi za kidini (Shura ya Maimamu, Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu, TEC nk.), Jukwaa la Wahariri, TLS, Raila Odinga wa Kenya, na Jaji Joseph Warioba ili kuwaeleza juu ya msimamo wao.
Lissu ameieleza mahakama kuwa shtaka la uhaini linalomkabili linatokana na maneno aliyoyazungumza tarehe 3 Aprili 2025 katika mkutano wa watia nia wa uchaguzi mkuu uliofanyika Makao Makuu ya CHADEMA Dar es Salaam. Mkutano huo uliandaliwa na Ofisi ya Katibu Mkuu wa chama na yeye alihutubia kama mzungumzaji mkuu kueleza msimamo wa chama, jambo ambalo ni wajibu wake kama Mwenyekiti.
Mwanasiasa huyo amefichua madai ya kushangaza kuwa upande wa mashtaka umewasilisha ushahidi wa video ya Jambo TV yenye urefu wa takribani saa tatu (au saa mbili kulingana na baadhi ya mashahidi), lakini yeye binafsi hajawahi kuiona wala kuoneshwa video hiyo tangu akamatwe mwaka jana kwasababu amekuwa akishikiliwa gerezani. Amesema kuwa maneno yanayodaiwa kuwa ni uhaini yakisomwa kwenye hati ya mashtaka hayazidi hata muda wa dakika moja, akishangaa kwanini maelezo yake ya masaa matatu yamefichwa.
Pia, Lissu amebainisha kuwa yeye siye aliyechapisha au kusambaza video hiyo. Ushahidi wa upande wa mashtaka kupitia Shahidi wa 17 (PW17) ulithibitisha kuwa Jambo TV ndio waliofanya matangazo ya moja kwa moja (Live coverage) kwenye YouTube, wakachapisha vipande vya video kupitia Instagram na X. ‘Coverage’ hiyo ilifanyika kufuatia mwaliko rasmi uliotolewa na Afisa Habari wa CHADEMA, Brendah Rupia, baada ya kupata idhini ya Mkurugenzi Mkuu wa Jambo TV.
Lissu amedai kuwa polisi na waendesha mashtaka walijua ukweli huu tangu tarehe 8 Aprili, lakini wakaamua kumtuhumu yeye kuchapisha na kumshtaki kwa uhaini ili kumweka gerezani kwa hila.
Katika utetezi wake, Lissu amefafanua kuwa katika mkutano huo na watia nia, alikuwa akiwaeleza kwa kina mfumo mbovu wa uchaguzi uliopo nchini Tanzania kwa miaka mingi. Amezungumzia kile alichodai kuwa ni uandikishaji mbovu wa wapiga kura, mbinu za kuwaengua wagombea wa upinzani, jinsi Tume ya Uchaguzi inavyoundwa na wateule wa Rais (ambaye ni Mwanaccm), na Wakurugenzi wa Halmashauri (ambao ni wasimamizi wa uchaguzi), vyombo vya dola, polisi, na watendaji vya vijiji kuwakandamiza wapinzani.
Lissu ameeleza kuwa CHADEMA iliona kuwa mfumo huo ungeleta maafa makubwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. Ndiyo maana, katika mkutano huo, Lissu alipendekeza kuwa ikiwa mabadiliko ya kikatiba na ya tume ya uchaguzi yanahitaji muda mrefu kutekelezwa, basi chama kipo tayari uchaguzi mkuu uahirishwe na viongozi waliopo madarakani waendelee kutawala, mradi tu mabadiliko hayo yafanyike kwa pamoja. Hata hivyo amedai kuwa serikali na CCM walikataa ushauri huo, wakalazimisha uchaguzi uliosababisha vifo vya mamia ya Watanzania.
Kuhusu matumizi ya neno “tutakinukisha”, “tutazuia uchaguzi”, au “tutavuruga uchaguzi”, Lissu amesema maneno hayo yalichomolewa nje ya muktadha. Amesisitiza kuwa kisheria hakuna kosa la jinai linaloitwa “kukinukisha”, “kuzuia uchaguzi”, au “kuvuruga uchaguzi”. Ameongeza kuwa nia yake haikuwa kuitishia serikali bali kuuhamasisha na kuelimisha umma kudai mabadiliko kwa amani.
Baada ya Lissu kumaliza kutoa sehemu hiyo ya utetezi wake, jopo la majaji liliafiki kuahirisha shauri hilo kutokana na muda wa mahakama kumalizika. Kesi imeahirishwa hadi siku ya Jumatano, tarehe 26 Agosti 2026, ambapo Tundu Lissu anatarajiwa kuendelea kushusha sehemu inayofuata ya utetezi wake akichambua ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na kuonyesha ikiwa unatosha “kunyonga mtu” au la.