Latest Posts

LISSU ADAI UKAMATAJI NA UPELEZI ULIKIUKA SHERIA/ ACHAMBUA DHANA YA KUITISHIA SERIKALI “NIMEMTISHIA NANI?

Kesi ya uhaini namba 19605/2025 inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Antiphas Lissu, Jumatano Agosti 26, 2026 imefikia hatua ya kusisimua baada ya mwanasiasa huyo kushusha utetezi wake wa mwisho.

Katika ushahidi wake uliodumu kwa masaa kadhaa mbele ya jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Dastan Ndunguru, Lissu ameeleza kuwa upelelezi wa kesi inayomkabili umefanyika “kienyeji” na kwa hila za kisiasa, huku akiwananga baadhi ya mashahidi wa upande wa mashtaka (mashahidi wa siri) akisema kuwa waligeuzwa kutoka kuwa wahalifu na kuwa mashahidi wa serikali.

Katika utetezi wake, Lissu aliwachambua mashahidi 17 walioletwa na upande wa mashtaka, kati ya 30 waliokuwa wameorodheshwa hapo awali. Lissu amebainisha kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuwaleta mashahidi 13, jambo ambalo alisema si la bahati mbaya bali lilikusudia kuficha ukweli wa ukamataji wake.

Amesema katika mashahidi 17 waliofika mahakamani mashahidi 8 walikuwa ni maafisa wa polisi wanaofanya kazi chini ya IGP Camilius Wambura na DCI Ramadhan Kingai, watu ambao Lissu ameeleza kuwa ana migogoro na chuki nao ya binafsi kwa takribani miaka 24 kutokana na harakati zake za kupinga ukandamizaji.

Amesema mashahidi 9 waliobaki walikuwa ni “mashahidi wa siri au kificho” ambao hawajulikani majina yao, makazi yao, wala kazi zao na mahakama au upande wa utetezi, isipokuwa na waendesha mashtaka pekee. Walipewa majina ya kificho kama PW1, PW2, nk.

Lissu amesema kuwa kupitia maelezo ya maandishi ya mashahidi hawa wa kificho (isipokuwa PW4), mashahidi 7 wa kificho walikiri kwa maandishi na kwa mdomo mahakamani kuwa walipanga njama za kufanya uhalifu wa kupiga watu na kuchoma moto majengo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025. Polisi waliwatambua na kuwakamata kati ya tarehe 4 na 8 Aprili 2025. Hata hivyo, badala ya kuwashtaki kwa makosa hayo mazito ya jinai na vurugu zilizosababisha vifo vya mamia ya raia, polisi waliwaachia huru kwa maelekezo ya PW16 (ACP Amini Mahamba). Baadaye, polisi waliwapa sharti: “Kubalini kuwa mashahidi dhidi ya Lissu, na tukifanya hivyo tutafuta mashtaka yenu.” Mashtaka yao yote yalifutwa baada ya kukubali mpango huo.

“Huu ndio ushahidi wa serikali dhidi yangu… ushahidi wa wahalifu waliokiri kwa maandishi, wakaachiwa huru wakati watu waliuawa kwenye uchaguzi. Ushahidi wa aina hii hauwezi kuwa salama hata kidogo (totally unsafe and unreliable),” amesema Lissu.

Lissu ameendelea kueleza juu ya upelelezi akirejea ushahidi wa PW1 (ACP George Bagyemu), Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Kanda ya Dar es Salaam (Deputy ZCO), ambaye aliongoza timu ya wapelelezi tangu tarehe 4 Aprili hadi 8 Aprili 2025 kabla ya ukamataji wa Lissu tarehe 9 Aprili 2025.

Lissu amesema katika mahojiano ya ana kwa ana (cross-examination), PW1 alikiri makosa makubwa ya kiupelelezi ikiwamo kutoshirikisha kabisa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambayo kisheria ndiyo yenye mamlaka ya kuratibu upelelezi wote wa jinai nchini, hakushirikisha kabisa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), licha ya kuwa hii ni kesi ya kwanza na kubwa zaidi ya uhaini nchini.

Zaidi ya hayo, PW1 alikiri kuwa yeye kama kiongozi mkuu wa upelelezi hakuamuru Lissu akamatwe na wala hakuwa anajua ni nani aliyeamuru ukamataji huo. Alipokea tu simu kutoka kwa DCP Ng’anzi kuwa Lissu amekamatwa mkoani Ruvuma na anasafirishwa usiku kucha kuletwa Dar es Salaam. Lissu anasema jambo hilo linathibitisha kuwa amri hiyo ilitoka juu moja kwa moja kwa chuki binafsi za IGP Wambura na DCI Kingai.

Halikadhalika, Lissu ameeleza jinsi alivyokamatwa tarehe 9 Aprili 2025 mjini Mbinga, mkoani Ruvuma, majira ya saa 12 jioni akimalizia kuhutubia mkutano wa hadhara. Ameeleza kuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mbinga (OCD), Lugano Gwasa, alipanda jukwaani na kumwambia: “Nataka kukuona sasa hivi.”

Lissu alipomuuliza kosa lake, OCD Gwasa alijibu: “Wewe twende, tutajua mbele ya safari.” Lissu alipokataa katakata kukamatwa bila kuelezwa kosa lake kinyume cha sheria, polisi walifyatua mabomu ya machozi jukwaani, kuwapiga raia marungu, na ghafla Lissu alijikuta ametupwa kwenye gari la polisi la Land Cruiser akiwa amekanyagwa shingo.

Baadaye alifikishwa kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mbinga (OCCID) ambaye alikiri kuwa walipokea amri tu kutoka kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) Marco Chilya bila kuelezwa kosa la Lissu. RPC Chilya naye alikiri kupokea maagizo kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma (kwa IGP Wambura) ya kumsafirisha Lissu usiku huo huo kwenda Dar es Salaam. Lissu alisafirishwa usiku kucha bila kula wala kupewa nafasi ya kupumzika na bila kujua kosa lake hadi kesho yake asubuhi alipofika Dar es Salaam.

Mwanasiasa huyo amehoji kwanini OCD Lugano Gwasa na RCO Charles Makunja walioorodheshwa kama mashahidi wa upande wa mashtaka walishindwa kuletwa mahakamani. Amesisitiza kuwa walifanya hivyo makusudi ili kukwepa kuumbuka kizimbani kuhusu ukamataji huo aliodai kuwa ulikiuka misingi yote ya haki za binadamu na taratibu za kisheria.

Kuhusu kiini cha shtaka lenyewe ambalo linahusu kauli alizozitoa tarehe 3 Aprili 2025 kwenye mkutano wa watia nia wa CHADEMA, Lissu amebainisha kile alichokieleza kama udhaifu mkubwa wa kisheria wa upande wa mashtaka

Amesema upande wa mashtaka unadai kuwa uthibitisho wa uhaini upo kwenye video iliyochapishwa kwenye Jambo TV yenye urefu wa takriban saa matatu. Hata hivyo, upande wa mashtaka umeshindwa kabisa kuwasilisha video hiyo kama kielelezo mahakamani. Lissu amesisitiza kuwa maneno matupu hayatengenezi kosa la uhaini (mere words do not constitute overt acts), na kukosekana kwa video hiyo kunamaanisha hakuna kesi ya uhaini.

Lissu amesema shahidi pekee aliyekuwepo kwenye mkutano huo na kusikia kauli za Lissu ni mwandishi wa habari PW17 (kupitia Kielelezo D16). PW17 alikiri mahakamani na kwenye maelezo yake ya polisi kuwa yeye ndiye aliyechapisha, kurusha ‘Live’ na kuhifadhi video hiyo kwenye mitandao ya Jambo TV akitumia kamera za NX. Alipoulizwa kama alisikia kauli yoyote ya jinai au uhaini kutoka kwa Lissu, PW17 alijibu “Hapana.”

Aidha, Lissu alielezea ushahidi wa PW2 (John Kaaya – Polisi). Katika Kielelezo D1, askari huyu alikiri kuwa aliona picha mjongeo yenye “viashiria vya jinai” lakini hakuna sehemu yoyote aliyotaja au kuona nia ya uhaini au kosa la uhaini. Lissu amehoji jinsi gani yeye anashtakiwa kwa “kuchapisha” maneno hayo wakati upelelezi wenyewe tangu tarehe 8 Aprili ulishafahamu kuwa mchapishaji alikuwa ni Jambo TV na mwandishi wao PW17.

Halikadhalika, Lissu amekichambua Kifungu cha 39(2d) cha Kanuni ya Adhabu kinachozungumzia “kuitishia serikali.” Ameeleza kuwa kifungu hiki ni kipana mno na hakitekelezeki katika mazingira ya sasa. Kikatiba, “Executive” (Serikali) inajumuisha viongozi kuanzia Rais hadi watendaji wa vijiji na mitaa. Lissu amehoji: “Kama nilitishia serikali, ni nani niliyemtishia? Kwenye kauli zangu zote, hakuna jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais Samia, Waziri Mkuu, IGP wala kiongozi yeyote wa serikali mtaa au kuu.”.

Pia, Lissu amedai ukiukwaji wa makusudi wa misingi ya kisheria wakati wa upelelezi kama kuvunjwa kwa Presumption of Innocence (Kudhaniwa Kutokuwa na Hatia). Amesema polisi waliona video tarehe 4 Aprili 2025 na siku hiyo hiyo wakaona kuna kesi ya uhaini bila kufanya upelelezi wa kina, bila kushauriana na wanasheria wa serikali, na bila kumhoji Lissu wala viongozi wa CHADEMA kupata maana ya kauli zao. Amesema walifanya upelelezi wakiwa tayari wanaamini kuwa Lissu ni mkosaji.

Aidha, Lissu amesema polisi mashahidi walikiri kufahamu Vifungu vya Kanuni ya Adhabu na Kifungu cha 52(2) cha Sheria ya Vyombo vya Habari, vinavyoeleza kuwa kukosoa serikali na sera zake kwa lengo la kuonyesha mapungufu au kutaka mabadiliko si kosa la jinai wala uchochezi. Hata hivyo, walivipuuza vifungu hivyo makusudi wakati wa upelelezi.

Lissu amehitimisha utetezi wake kwa kuonesha jinsi ushahidi wa maandishi wa polisi ulivyo batili kisheria. Ameeleza kuwa Askari polisi 7 (PW1, PW2, PW3, PW6, PW9, PW12 na PW16) waliandika maelezo yao wenyewe ya polisi na kuyathibitisha (kuyasaini) wenyewe (self-witnessed/self-certified) kinyume kabisa na utaratibu wa kisheria unaotaka maelezo ya shahidi yaandikwe mbele ya askari mwingine huru. Ni askari mmoja tu (PW15) aliyefuata sheria hiyo.

Kutokana na hilo, Lissu amesema kuwa mashahidi wote 17 wa upande wa mashtaka wametoa ushahidi wa mdomo kizimbani ambao unapingana na maelezo yao ya maandishi waliyoyaandika polisi, huku wakiongeza mambo mapya ambayo hawakuwahi kuyaandika hapo awali.

Baada ya Lissu kumaliza kutoa ushahidi wake wa utetezi, jopo la majaji limeahirisha kesi kwa ajili ya mapumziko ya kiafya hadi saa 8:30 mchana, ambapo mwanasiasa huyo anatarajiwa kurejea kizimbani kuanza kukabiliwa na maswali ya dodoso kutoka kwa jopo la mawakili wa serikali wakiongozwa na Nassor Katuga

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!