Kesi ya uhaini namba 19605/2025 inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Antiphas Lissu, inaendelea leo Jumanne, Septemba 1, 2026, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ambapo Katibu Mkuu wa chama hicho, John John Mnyika, anaendelea kukabiliana na maswali makali ya dodoso kutoka kwa mawakili wa serikali.
Katika siku ya leo, mawakili wa upande wa mashtaka (Jamhuri) walijaribu kuunganisha msimamo wa kisiasa wa CHADEMA wa “No Reforms No Election” na vitendo vya vurugu vilivyotokea wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana, huku Mnyika akisimama kutetea haki ya kupinga uchaguzi aliouita haramu kwa njia za kidemokrasia.
Wakili wa Serikali Mkuu, Nassor Katuga alianza kumhoji Mnyika kuhusu ushiriki wake katika kutoa maoni mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria. Mnyika alikiri kuwa yeye ndiye aliyewakilisha chama kutoa maoni hayo. Mnyika alieleza kuwa alizuiliwa kutoa maoni kuhusu mabadiliko ya kikatiba kabla ya mabadiliko ya sheria mbele ya kamati hiyo, na kuongeza kuwa maoni yote ya mabadiliko ya kikatiba yalikataliwa.
Upande wa serikali ulipodai kuwa kukataliwa kwa maoni hayo kulisababisha CHADEMA kurudisha “mpango mkakati wa kuzuia uchaguzi,” Mnyika alipinga vikali hoja hiyo akisema “hutakuwa sahihi,” ingawa alikiri kuwa mpango wa kuzuia uchaguzi usio huru ulikuwa ni mkakati rasmi wa chama
Upande wa mashtaka ulijaribu kuhoji uhalali wa mkutano wa watia nia wa Aprili 3, 2025, uliosababisha kesi hiyo. Jamhuri ilihoji mkutano rasmi unavyoweza kuendeshwa bila kuwa na Mwenyekiti, bila kumbukumbu (minutes), na bila ajenda. Mnyika alifafanua kuwa chama chao kina mikutano yenye wenyeviti na isiyo na wenyeviti kulingana na aina ya mkutano. Aliongeza kuwa mkutano huo haukuwa na ajenda rasmi bali ulikuwa na “mada” maalumu ya “No Reform No Election” kwa ajili ya kuwaelimisha na kusikiliza mawazo ya watia nia
Mvutano uliendelea pale upande wa mashtaka ulipojaribu kumwambia Mnyika kutoa tafsiri ya neno “ajenda” na “mada” kwa kutumia kamusi. Mnyika alisoma tafsiri ya kamusi inayofafanua ajenda kama “orodha ya mada zitakazojadiliwa kwenye mkutano,” na mada kama “jambo linalozungumzwa au kujadiliwa”. Alisisitiza kuwa maneno hayo ni tofauti kisheria na kiutendaji.
Sehemu kubwa ya dodoso ilijikita kwenye tafsiri ya neno “uasi” linalodaiwa kutumiwa na Lissu. Upande wa mashtaka ulitaka kujua kama tafsiri ya Mnyika ya neno uasi inatokana na kauli ya Mwalimu Nyerere aliyewahi kusema anapenda kuona vijana wakiasi dhidi ya mifumo kandamizi. Mnyika alijibu “si kweli” na kueleza kuwa uelewa wake wa neno uasi kiasili ni “kukataa na kupinga kwa nguvu kubwa sana”
Alipobanwa kueleza maana ya kuhamasisha uasi dhidi ya uchaguzi, Mnyika alijibu kuwa “Ni kukataa uchaguzi usio wa haki, wa halali, usio huru”. Alisisitiza kuwa kuhamasisha uasi na kuzuia uchaguzi kwa “nguvu zote za kidemokrasia” ni njia halali ya kisiasa na kidemokrasia. Aliongeza kuwa vyama vingine vina haki ya kushiriki uchaguzi huru na wa haki, lakini “havikuwa na haki ya kushiriki uchaguzi haramu”
Mnyika alifafanua kuwa kauli za Tundu Lissu kama vile “tutakinukisha” na “tutaenda kuzuia uchaguzi” zililenga kutaka mabadiliko ya kisheria na kikatiba yafanyike. Hata hivyo, alikataa madai ya serikali kuwa maneno hayo yalilenga “kushinikiza” serikali kwa nguvu
Wakili wa Serikali alimbana Mnyika kuhusu ripoti ya Tume ya Jaji Chande iliyohusisha vurugu za tarehe 29 Oktoba 2025 na ushawishi wa wanasiasa kwa vijana. Mnyika alijibu kwa msisitizo: “Sikubaliani, na CHADEMA haikubaliani na tume ya Jaji Chande ya matukio ya Oktoba 29, 2025”. Alieleza kuwa walisikia tu hotuba hiyo lakini kusikia haimaanishi kukubali, na ndiyo maana CHADEMA ilihitaji tume huru ya uchunguzi ya kimataifa.
Alikana kuwa maneno ya Lissu yanafanana na yaliyoelezwa kwenye ripoti hiyo, akisema: “Mwenyekiti hakuhusika kabisa na kuhamasisha uasi kwa vurugu”. Mnyika alikiri kuwa aliona uharibifu wa baadhi ya miundombinu kama vile vituo vya mwendokasi jijini Dar es Salaam lakini akabainisha kuwa kuzuia uchaguzi kwa njia ya kidemokrasia ni pamoja na kususa kura na kuruhusu wengine wapige bila kufanya vurugu
Hata hivyo, maswali ya dodoso kwa Mnyika kwa mchana wa leo hayakumalizika baada ya jopo la majaji kuingilia kati na kuahirisha kesi hiyo hadi saa nane na nusu mchana wa leo Septemba 1, 2026 ili maswali ya dodoso yaweze kuendelea.